Chameleone atua Dar, aahidi makubwa bongo fleva honors
Muktasari:
- Chameleone amewasili akiwa ameambatana na mama yake mzazi pamoja na bendi yake nzima, akionesha utayari wa kutoa burudani ya kiwango cha juu katika tamasha hilo linalotarajiwa kukutanisha mastaa mbalimbali wa muziki wa Tanzania.
MSANII nguli wa muziki kutoka Uganda, Jose Chameleone amewasili nchini Julai 27, 2026, tayari kushiriki tamasha la Bongo Fleva Honors litakalofanyika Julai 31, 2026, katika Ukumbi wa SuperDome, Masaki, Dar es Salaam.
Chameleone amewasili akiwa ameambatana na mama yake mzazi pamoja na bendi yake nzima, akionesha utayari wa kutoa burudani ya kiwango cha juu katika tamasha hilo linalotarajiwa kukutanisha mastaa mbalimbali wa muziki wa Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Chameleone amesema anafurahia kurejea Tanzania na kushiriki tamasha hilo, akieleza kuwa amejiandaa kuwapa mashabiki onyesho litakalobaki kwenye kumbukumbu zao.
"Ninafurahi kuwa Tanzania tena. Nawashukuru waandaaji kwa kunipa heshima hii. Watu wengi wamekuwa wakinisikiliza kwa miaka mingi lakini sasa wataniona jukwaani nikiwa na bendi yangu kamili. Ninaamini itakuwa shoo ambayo mashabiki wataikumbuka kwa muda mrefu," amesema Chameleone.
Amesema Tanzania ni moja ya nchi zilizochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya muziki wake, hivyo aliamua kuja na bendi yake yote ili kuwapa mashabiki burudani ya kiwango cha kimataifa na kuwashukuru kwa sapoti waliompa kwa miaka mingi.
Kwa upande wake, msanii na mwanasiasa amesema uwepo wa Chameleone katika Bongo Fleva Honors ni heshima kubwa kwa tamasha hilo, akieleza kuwa msanii huyo amekuwa na mchango mkubwa katika kukuza muziki wa Afrika Mashariki na kuimarisha uhusiano wa muziki kati ya Tanzania na Uganda.
"Mchango wa Jose Chameleone katika muziki wa Bongo Fleva ni mkubwa sana. Ni mmoja wa wasanii wa nje walioweza kufanya ziara nyingi za muziki katika mikoa mbalimbali ya Tanzania kuliko hata baadhi ya wasanii wa hapa nyumbani. Amechangia kwa kiasi kikubwa kuukuza muziki wa Afrika Mashariki, ndiyo maana tumeona anastahili kuwa sehemu ya Bongo Fleva Honors," amesema Sugu.
Sugu ameongeza kuwa Chameleone ameandika historia kwa kuwa msanii wa kwanza kutoka nje ya Tanzania kushiriki Bongo Fleva Honors, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaonesha namna muziki wa Bongo Fleva ulivyovuka mipaka na kuendelea kuunganisha wasanii wa Afrika Mashariki.
"Huyu ndiye msanii wa kwanza wa kimataifa kushiriki Bongo Fleva Honors, lakini naamini hatakuwa wa mwisho," amesema.