Celine Dion aonekana baada ya miaka miwili
Muktasari:
- Nyota huyo mwenye umri wa miaka 58 alionekana wakati akijiandaa kurejea jukwaani, ambapo alitabasamu huku akiwa amevalia mavazi ya mtindo wa kuvutia yakiambatana na jaketi la ngozi ya kahawia lenye mwonekano wa ngozi ya mamba pamoja na suruali nyeusi aina ya culottes.
PARIS, UFASANSA: CELINE Dion, mwanamuziki mkongwe wa R&B ameonekana akiwa katika hali nzuri na mwenye furaha alipokuwa akiwapungia mashabiki wakati akiondoka katika Hoteli ya Royal Monceau jijini Paris, Ufaransa, ikiwa ni baada ya miaka miwili kupita.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 58 alionekana wakati akijiandaa kurejea jukwaani, ambapo alitabasamu huku akiwa amevalia mavazi ya mtindo wa kuvutia yakiambatana na jaketi la ngozi ya kahawia lenye mwonekano wa ngozi ya mamba pamoja na suruali nyeusi aina ya culottes.
Mwanamama huyo alikamilisha mwonekano huo kwa buti nyeusi za ngozi zenye visigino na miwani ya jua. Celine sasa anajiandaa kurejea jukwaani miaka mitatu baada ya kulazimika kusitisha ziara yake ya dunia kutokana na mapambano makali dhidi ya tatizo la kiafya linalofahamika kama Stiff Person Syndrome (SPS), ugonjwa adimu wa mfumo wa neva unaosababisha kukakamaa kwa misuli na maumivu pamoja na mikazo ya misuli.
Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, Celine ametumbuiza hadharani mara moja pekee, na aliwahi kueleza kwa undani ukali maumivu katika filamu yake ya mwaka 2024, “I Am: Celine Dion.”
Kuonekana kwake hadharani mara ya mwisho kulikuwa mwaka huohuo alipokuwa akiimba katika tukio la mitindo la Elie Saab jijini Riyadh, Saudi Arabia. Hata hivyo, tangu wakati huo ameonekana akiwa miongoni mwa watazamaji katika matamasha ya Paul McCartney na Coldplay.
Mwezi Machi, Celine alitangaza kurejea jukwaani kwa ajili ya maonyesho 10 jijini Paris yatakayoanza msimu huu. Kutokana na mahitaji makubwa kutoka kwa mashabiki, ameongeza maonyesho mengine 16 yatakayofanyika kuanzia Septemba mwaka huu hadi Mei 2027.
AJIANDAA KWA MAZOEZI MAKALI
Celine alizungumza mwezi uliopita kuhusu maandalizi yake ya kurejea jukwaani, pamoja na hofu na hali ya kutojiamini ambayo amekuwa akijifunza kuikabili tangu kugundulika kwa tatizo hilo.
Mwimbaji huyo amekuwa akijiandaa kwa maonyesho yake kwa ratiba kali ya mazoezi inayojumuisha vipindi vya dakika 90 mara tatu kwa wiki, pamoja na mazoezi ya mara mbili kwa wiki akiwa na kampuni ya moja maarufu kwa ajili ya kazi hiyo.
“Ni hali inayoendelea hatua kwa hatua. Sipendi kusema ‘ugonjwa’. Neno ugonjwa linakufanya ufanye hivi,” alisema huku akikunjakunja pua yake.
Mahojiano yalifanyika katika studio ya kurekodia iliyopo Palms Casino Resort, chumba kilichokuwa na vifaa mbalimbali vya mazoezi, vikiwemo uzito, mashine ya kukimbilia, ya reformer na nguzo ambayo Dion alikuwa akiitumia kujinyoosha.
Baada ya miaka kadhaa ya kukumbwa na dalili, Celine aligundulika kuwa na SPS 2022, baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya 2020 kipindi ambacho pia kilikuwa mwanzo wa janga la Uviko. Kwa takribani miaka mitatu, alijitenga na mashabiki, kwa sehemu kutokana na hofu kwamba mashabiki wake wangefikiri anaishi maisha yenye furaha, lakini bado anaendelea kutofanya maonyesho yake.
Katika kipindi hicho pia alianza kuthamini zaidi mazingira na asili. “Napenda sana miti, na nilikuwa na picha akilini mwangu ya kujificha na kutoweka kupitia kwenye majani,” alikaririwa akisema.
Miti hiyo ilikuwa haina majani kwa sababu ulikuwa msimu wa vuli, hali ambayo Dion aliiona kama mfano wa changamoto alizokuwa akipitia.
“Nilikuwa nikijaribu kuwaambia, samahani, sina tena maajabu ya kuwapa; tulikuja kwa ajili ya mti,” alisema.
Mara ya mwisho Celine kutumbuiza jukwaani ilikuwa katika Michezo ya Olimpiki Paris 2024, na sasa anajiandaa kurejea jukwaani akiwa na ratiba nzito ya mazoezi, katika kipindi anachokielezea kama maisha ya kuanguka na kuinuka tena na tena.
“Umekuwa muda mrefu sana. Ningependa kuwapa kitu kitakachoonyesha jinsi nilivyowakosa,” alisema.
MAONYESHO 10 JIJINI PARIS
Mwezi Machi, mwanamuziki huyo alitangaza kwamba atafanya maonyesho 10 katika Paris La Defense Arena, ukumbi wenye uwezo wa kuchukua watu 40,000, katika miezi ya Septemba na Oktoba. Alitangaza kurejea kwake siku ya kuzaliwa kwake na kuelezea tukio hilo kama “zawadi bora zaidi ya maisha yangu.”
Katika video aliyoweka mitandaoni alisema: “Niko tayari sana kufanya hivi. Najisikia vizuri, nina nguvu, nahisi msisimko bila shaka, na pia nina wasiwasi kidogo. Naendelea vizuri, nasimamia afya yangu, najisikia vizuri. Naanza tena kuimba hata kucheza kidogo.
“Lakini lazima niwaambie jambo muhimu sana; katika miaka hii yote iliyopita kila siku iliyopita nimekuwa nikihisi maombi yenu na msaada wenu, wema wenu na upendo wenu. Nawashukuru sana nyote. Siwezi kusubiri kuwaona tena.”
Baadaye aliongeza tarehe nyingine kutokana na “mahitaji makubwa kutoka kwa mashabiki,” akiongeza maonyesho 10 zaidi mwezi Mei.
SPS ILIVYOBADILISHA MAISHA YAKE
Stiff Person Syndrome ni ugonjwa adimu wa mfumo wa neva unaosababisha kukakamaa kwa misuli na mikazo yenye maumivu inayoweza kutokea na kutoweka, huku hali hiyo ikizidi kuwa mbaya kadiri muda unavyokwenda, na Celine amewahi kueleza jinsi ugonjwa huo ulivyoathiri hata sauti yake ambayo ndiyo alama yake katika muziki.
Mwimbaji huyo alitangaza kwa mara ya kwanza 2022 kwamba alikuwa akisumbuliwa na SPS na wakati huo alilazimika kuacha maonyesho yaliyokuwa yamesalia katika ziara yake.
Katika video aliyoweka kwenye ukurasa wake wa Instagram wakati huo, Celine alisema kwa hisia: “Kwa bahati mbaya, mikazo hii inaathiri kila sehemu ya maisha yangu ya kila siku. Wakati mwingine inanifanya nipate ugumu wa kutembea na hainiruhusu kutumia kamba zangu za sauti kuimba kama nilivyozoea.”
“Ninafanya kazi kwa bidii kila siku na mtaalamu wangu wa tiba ya michezo ili kujenga tena nguvu zangu na uwezo wangu wa kutumbuiza, lakini lazima nikiri kwamba imekuwa changamoto. Kitu pekee nachokijua ni kuimba. Nimefanya hivyo maisha yangu yote, na ndicho kitu nachokipenda zaidi kufanya,” alisema mama huyo wa watoto watatu.
Mwezi Mei 2024, Celine alitoa taarifa kuhusu afya yake katika mahojiano na Vogue, akisema kwamba “furaha yangu imerudi. Imekuwa mzigo mkubwa mabegani mwangu, na sehemu kubwa ya uzito huo imeondoka... kwa sababu sasa naweza kuangazia uhalisia. Hilo ni jambo zuri.”
Mwimbaji huyo alisema anaamini ndani yake na ujasiri wake, akisisitiza kwamba hataruhusu ugonjwa huo “utawale maisha yangu.”