BONGO MUSIC FACTS: Belle 9 naye kama Dully Sykes na Juma Nature
Muktasari:
- Akiwa ametoa EP moja, Baba Boss TV (2022), Belle 9 ametengeneza nyimbo nyingi kubwa kwa zaidi ya miaka 10 na kushirikishwa na wasanii wengi hasa wale wa Hip Hop na kolabo hizo kufanya vizuri. Fahamu zaidi.
MWIMBAJI Belle 9 jina lake lipo kwenye orodha ya wakali wa RnB hapa nchini kwa muda wote. Sauti yake, melodi, uandishi na swaggs ni miongoni mwa mambo yanayomfanya kuendelea kuwepo katika muziki.
Akiwa ametoa EP moja, Baba Boss TV (2022), Belle 9 ametengeneza nyimbo nyingi kubwa kwa zaidi ya miaka 10 na kushirikishwa na wasanii wengi hasa wale wa Hip Hop na kolabo hizo kufanya vizuri. Fahamu zaidi.
1. Wimbo wa kwanza kwa Belle 9 kutoa sio 'Sumu ya Penzi' kama wengi wanavyojua, kabla ya 'Sumu ya Penzi' alishatoa nyimbo nyingine kama 'Mrembo', 'Mrembo wa Kiafrika Remix' na 'Kaja na Nani', na hizi zilipata kusikika tu mkoani kwao Morogoro.
2. Kabla ya Belle 9 kuanza kusikika akiimba muziki mzuri wa RnB, mwanzo kabisa alikuwa akichana, yaani rap. Pia utakumbuka kuna waimbaji wazuri Bongo kama Jux, Diamond Platnumz, Vanessa Mdee, Aika, Dayna Nyange na Dully Sykes waliaza kwa kuchana.
3. Shoo ya kwanza ya Belle 9 kulipwa fedha nyingi alitumbuiza pamoja na Dayna Nyange mkoani Morogoro na kutokana na fedha alizozipata aliamua kuacha kazi aliyokuwa akiifanya kwenye kiwanda cha Tumbaku na kuingia rasmi katika muziki.
4. Video ya kwanza kwa Belle 9 kugharimu fedha nyingi ni ya wimbo wake 'Shauri Yao' ambayo alitoa Sh12 milioni ambapo Director pekee, Hanscana alichukua Sh4 milioni na hii ndio video ya kwanza kufanyika chini ya lebo yake, Vitamini Music Group (VMG).
5. Kuna nyimbo kadhaa Belle 9 alizoshirikishwa na wasanii wengine Bongo lakini kwenye video zake hajaonekana, video hizo ni 'Vuvuzela' ya Baba Levo, '13' ya Young Killer na 'Tunasafisha' ya Edu Boy.
Hiyo ni sawa na Jux, mkali mwingine wa RnB ambaye hajaonekana kwenye video za wenzake kama 'Pesa Yangu' ya Lord Eyes, 'Mtu Tatu' ya kundi la Mtu Chee na 'Sirudi Tena' ya Mabeste.
6. Wimbo wa Belle 9 'Give It To Me' amechukua vionjo kutoka kwenye wimbo 'Maria Salome' wake Saida Karoli, nyimbo nyingine za Bongofleva zilizofanya hivyo ni 'Salome' wake Diamond Platnumz na 'Muziki' wake Darassa.
7. Mwimbaji Bruno Mars kutokea Marekani ndiye msanii ambaye akitoa wimbo lazima Belle 9 autafute na kuusikiliza. Hii ni kutokana msanii huyo ana uwezo wa kuimba kwa sauti ya juu, pia muziki wake una vitu vingi vya kisasa na vionjo vya zamani.
8. Wimbo wa Belle 9 'Burger Movie Selfie Remix' ndio wimbo wenye vitu vingi zaidi kutoka kwake, kwanza umepita kwenye mikono ya maprodyuza wanne ambao ni Ema The Boy, Tudd Thomas, Chizan Brain na Tiddy Hotter. Pili video yake iliyotoka Juni 25, 2016 imesimamiwa na waongozaji watatu ambao ni Khalfan, Hanscana pamoja na Enos Olik kutokea Kenya.
9. Video ya wimbo wa Belle 9 'Give It To Me' ndio ya kwanza kwake kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 1 YouTube, video hiyo ilitoka Desemba 17, 2016 na ilifanyika Afrika Kusini, pia ndio video ya kwanza kwa Belle 9 kufanya nje ya Tanzania.
10. Licha ya kutoa nyimbo kali na maarufu, hadi sasa Belle 9 hajawahi kushinda tuzo yoyote ya muziki Tanzania (TMA) kama ilivyo kwa kaka zake kimuziki, Dully Sykes, Juma Nature, Mr. Blue na kadhalika.
Hata hivyo, utakumbuka Belle 9 ndiye aliyeimba kiitiko cha wimbo uliomtoa Young Killer 'Dear Gambe' na kumuwezesha kushinda tuzo ya kwanza na ya pekee hadi sasa kutoka TMA kama Msanii Bora Chipukizi 2014.