BONGO MUSIC FACTS: Baada ya Best Naso, anafuata Rayvanny!
Muktasari:
- Tayari ametoa albamu tatu ambazo ziliuza kwa kiwango fulani na kumpatia fursa nyingine za kimuziki ila kwa kipindi chote alichofanya vizuri hadi sasa hakuwahi kushinda tuzo yoyote. Songa nayo.
Hadi sasa Best Naso yupo katika orodha ya vipaji vikubwa kutoka Kanda ya Ziwa zilivyoishika Bongo Fleva kwa kipindi fulani, huku aina ya utunzi wake wenye kubeba ujumbe ukimpatia umaarufu.
Tayari ametoa albamu tatu ambazo ziliuza kwa kiwango fulani na kumpatia fursa nyingine za kimuziki ila kwa kipindi chote alichofanya vizuri hadi sasa hakuwahi kushinda tuzo yoyote. Songa nayo.
1. Hadi kuja kugundua ana kipaji cha muziki ilikuwa mwaka 1997 alipoenda Moshi, Kilimanjaro sehemu moja inayoitwa Nyumba ya Mungu kwa shangazi yake, huko alikutana na vijana wanarap, wakawa wanamwandikia mistari halafu anachana tu.
2. Baadaye kuna wimbo wa Mabaga Fresh unaitwa 'Tunataabika' ulitoka, kutokana na ule wimbo, ndiyo kwa mara ya kwanza kabisa akaandika mistari yake kutokana na melodi zake na kisha akaandika wimbo wake wa kwanza, Kilema.
3. Mwaka 2004 alirekodi wimbo wake wa kwanza 'Kilema' kwa Prodyuza Mchopa ambaye studio yake ilikuwa Banana, Dar es Salaam, ingawa kabla ya hapo alirekodi wimbo 'Sinyorita' kupitia kinanda tu kwa usaidizi wa Benja anayefanya muziki wa Injili.
4. Alilipa Sh15,000 kurekodi wimbo huo ila haikuwa ndio bei halisi ya kurekodi bali aliomba kusaidiwa maana alikuwa bado ni kijana wa nyumbani tu ambaye hana kazi, hivyo hata kupata kiasi hicho ilibidi kupambana sana.
5. Kisa alichoimba Best Naso katika wimbo wake, Mamu wa Dar (2009) ni cha kweli na si cha kubuni kama ambavyo watu wanaweza kudhani, bali ni simulizi aliyoisikia kwa masikio yake na kuamua kuileta kwa jamii kupitia muziki.
Huyo Mamu wa Dar ni mama wa rafiki yake ambaye anaishi Ubungo Maziwa, alikuwa akimsimulia jinsi ilivyokua hadi akamzaa huyo rafiki yake akiwa bado mwanafunzi hali iliyosababisha kushindwa kuendelea na shule.
6. Na wimbo huo, Mamu wa Dar (2009) ndio uliobeba jina la albamu yake ya kwanza ambayo mauzo yake yalifikia Sh6 milioni ila hadi sasa hakuna data kamili zinazoeleza albamu hiyo iliuza nakala kiasi gani kwa muda wote.
Fedha nyingi alizipata pindi albamu tu ilipotoka ila alipokuja kugonga kopi kwa mara ya pili akapata Sh700,000, na kwa mara ya tatu akapata Sh300,000.
7. Albamu yake ya pili, Narudi Kijijini (2013) ilifanya vizuri kutokana na umaarufu wa wimbo huo lakini kwa upande wa mauzo mambo hayakuwa mazuri kwani alipata takribani Sh2 milioni tu katika mradi wote huo!.
8. Licha ya mauzo yake kiduchu ila albamu hiyo ilifanya vizuri na kumpatia shoo za nje ya nchi kwa mara ya kwanza na alienda kutumbuiza huko DR Congo na alilipwa vizuri ukilinganisha na shoo za ndani.
9. Na albamu yake ya tatu, The Gift of Life (2021), ndiyo albamu iliyotoka mwaka 2021 ikiwa na nyimbo nyingi zaidi ambazo ni 32, hii ilipindua meza mbele ya ile ya Rayvanny, Sound From Africa (2021) ambayo ilitangulia kutoka ikiwa na nyimbo 23.
10. Licha ya muziki wake kufanya vizuri katika jamii, hadi sasa Best Naso hajawahi kushinda tuzo yoyote hata zile za muziki Tanzania (TMA) zinazoandaliwa na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) ikiwa ni sawa na Dully Sykes, TID, Mr. Blue, Juma Nature, Belle 9 n.k.
Utakumbuka tuzo za TMA ambazo zimekuwepo tangu mwaka 1999, hadi sasa wasanii walioshinda mara nyingi zaidi ni Diamond Platnumz, Alikiba na Lady Jaydee, mwanamuziki aliyetoa albamu tisa katika miaka yake 25 ndani ya Bongo Fleva.