Arobaini ya Sandrah: Matukio saba yaliyotikisa hafla
Muktasari:
- Mbali na kuwa siku ya kumsherehekea mtoto, hafla hiyo ilijaa matukio mbalimbali yaliyowafanya wageni na waliokuwa wakifuatilia kupitia mitandao ya kijamii kuendelea kuzungumzia kilichotokea usiku huo.
SHEREHE ya Arobaini ya mtoto wa Diamond Platnumz na Zuchu, Sandrah Naseeb, iliyofanyika Septemba 12 katika ukumbi wa St. Laurent Garden, Kawe jijini Dar es Salaam, ilikuwa miongoni mwa hafla zilizovuta hisia kubwa.
Mbali na kuwa siku ya kumsherehekea mtoto, hafla hiyo ilijaa matukio mbalimbali yaliyowafanya wageni na waliokuwa wakifuatilia kupitia mitandao ya kijamii kuendelea kuzungumzia kilichotokea usiku huo.
KUINGIA KUKACHELEWA
Tukio la kwanza lilianza kabla hata sherehe haijaanza rasmi, baada ya wageni kuchelewa kuingia ukumbini.
Waandishi wa habari pamoja na baadhi ya wageni waalikwa walikaa nje kwa muda mrefu wakisubiri kuingia, hali iliyodaiwa kusababishwa na mpambaji kuchelewa kufika kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mapambo.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya waliokuwa wamefika mapema kusubiri nje kwa takribani saa tano kabla ya kuanza kuingia ndani, ikiwa waliambiwa kuwasili saa 9 kamili.
DIAMOND AINGIA KWA KING’ORA
Baada ya kusubiri kwa muda mrefu, hatimaye majira ya saa mbili usiku, Diamond Platnumz aliwasili ukumbini kwa staili yake.
Diamond aliingia kwa kutumia king’ora akiwa ameongozana na mkewe Zuchu pamoja na watoto wake, huku ujio huo ukiwa miongoni mwa matukio yaliyovuta macho ya wageni.
RUBY NA RUSHAYNA MEZA MOJA
Tukio lingine lililovuta hisia katika hafla hiyo ni waliowahi kuwa wake wa Haji Manara, Rubyna na Rushayna, kuwekwa kwenye meza moja.
Kukaa kwao pamoja kwenye meza moja kulikuwa miongoni mwa mambo yaliyowafanya wageni kuzungumza, kutokana na historia yao ya kuwa waliwahi kuwa wake wenza na kulikuwa na madai kwamba hawaelewani.
BIRIANI IKAWA TATIZO
Upande wa chakula nao haukukosa tukio. Biriani, ambayo ilikuwa miongoni mwa vyakula vilivyotolewa, ilifika hatua ya kuisha wakati bado kulikuwa na wageni waliokuwa hawajapata chakula.
Baadhi ya waliopata katika awamu za mwisho walidaiwa kupewa biriani bila nyama wala rosti yake, jambo lililoacha baadhi ya wageni wakizungumza.
WAGENI WAKAKOSA VITI
Idadi ya wageni pia ilifanya baadhi yao kukosa nafasi za kukaa.
Wengine walijikuta wakisimama kwa sababu sehemu iliyotengwa kukaa watu haikutosha, hali iliyowafanya baadhi yao kukaa sakafuni.
Hali hiyo ilifanya baadhi ya wageni kusimama hadi mwisho wa tukio.
DIAMOND NA WASAFI HAWAKUPIGWA
Jambo jingine lililozua mshangao ni kutopigwa kwa wimbo hata mmoja wa Diamond Platnumz wala wasanii wengine wa Wasafi.
Badala yake, burudani kubwa ilitawaliwa na muziki wa taarabu na Kibao Kata.
Khadija Kopa, Sabaha Salum Muchacho pamoja na Jahazi Modern Taarabu ya Mzee Yusuf walitoa burudani hiyo, huku upande wa Bongo Fleva ukiwakilishwa na Kassim Mganga na singeli ikipata nafasi kupitia Dulla Makabila.
Hivyo, licha ya kuwa ilikuwa hafla ya Diamond na Zuchu, nyimbo za Diamond mwenyewe na Wasafi hazikusikika katika burudani ya usiku huo.
MIMI MALU NA DULLVAN WAKUTANA
Na kama haitoshi, 40 hiyo iliwakutanisha tena waliowahi kuwa wapenzi, Mimi Malu na Dullvan.
Wawili hao walionekana kuwa pamoja katika nyakati tofauti ndani ya hafla hiyo na kutumia muda pamoja.
Kukutana kwao kulivuta macho ya baadhi ya wageni kutokana na historia ya uhusiano wao, ambao uliwahi kuvunjika na Mimi Malu kuzungumzia kuvunjika kwa penzi hilo katika baadhi ya vyombo vya habari. Hivyo, uwepo wao pamoja katika hafla hiyo ukawa miongoni mwa matukio yaliyoipa 40 hiyo stori nyingine ndani ya stori.
Kwa ujumla, arobaini ya Sandrah haikuwa tu hafla ya kifamilia ya kumsherehekea mtoto, bali pia ilijaa matukio yaliyofanya usiku huo uzungumzwe kwa namna tofauti, kuanzia kuchelewa kwa wageni kuingia, ujio wa Diamond na familia yake, watu waliokutana baada ya historia zao za mahusiano, hadi burudani iliyotawala usiku huo.