Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AHMED MBARAKA; Safari yake kuwa mwonjaji wa taifa, alivyokutana na Wema Sepetu

Muktasari:

  • Huyu si mwingine bali ni Ahmed Mbaraka Ahmed, maarufu kama Mwonjaji wa Taifa, kijana mwenye shahada ya uzamili ambaye ameamua kutumia elimu na mitandao ya kijamii kusaidia biashara za watu, huku akitengeneza chapa inayotikisa kwa sasa.

KUPITIA kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram na TikTok, hivi sasa utakuwa unakutana na video za kijana mmoja mchangamfu, akionja vyakula mbalimbali na kuvitangaza kwa namna ya kipekee.

Huyu si mwingine bali ni Ahmed Mbaraka Ahmed, maarufu kama Mwonjaji wa Taifa, kijana mwenye shahada ya uzamili ambaye ameamua kutumia elimu na mitandao ya kijamii kusaidia biashara za watu, huku akitengeneza chapa inayotikisa kwa sasa.

Mwonjaji wa Taifa amefunguka mambo mengi kuhusu safari, siri ya kumpelekea pweza staa wa filamu, Wema Sepetu na changamoto kubwa zinazomkabili katika kazi yake hiyo ya kipekee.


WAZO LILIPOANZIA

Unajua wazo la kuonja vyakula lilianzia wapi? Ahmed anajibu akisema: “Njaa kali. Ndiyo ukiwa na njaa ubongo hufanya kazi kwa haraka sana kutafuta suluhisho na kwa kuwa kula ni hitaji la kila binadamu niliona kuna fursa kubwa hapo.”

Kabla ya kuwa maarufu, Ahmed anasema alikuwa akifanya maudhui kwa kuwasaidia wafanyabiashara barabarani bila kulipwa, akiamini kuwa elimu ni kitu cha thamani kinachopaswa kuwafikia wengi.

Safari yake ilichukua sura mpya alipofanya mahojiano na bibi mmoja maeneo ya Zanzibar aliyekuwa anauza urojo. Video aliyorekodi ilikwenda mbali zaidi na siku aliporudi Zanzibar yule bibi kwa furaha alimwambia aonje kila kitu kwenye meza yake.

Anasema hapo ndipo lilipozaliwa jina la “Mwonjaji wa Taifa wa Maslahi Mapana ya Taifa” kwa sababu akishaonja taifa linafahamu na maslahi yanapatikana kwa wafanyabiashara.

Moja ya matukio yaliyowahi kusisimua mitandao ni video yake akimpelekea pweza msanii maarufu wa Bongo Movie, Wema Sepetu baada ya kujifungua.

Ahmed anafichua kuwa lengo halikuwa kiki ya Wema, bali lilikuwa kumsaidia kijana muuza samaki barabarani maeneo ya Survey jijini Dar es Salaam. “Mba-raka alikuwa muuza samaki mzuri, lakini hakuwa anajua nguvu ya mitandao ukurasa wake wa Instagram ulikuwa na wafuasi 17 tu,” anasema.

Ahmed anasema aliamua kumsaidia wakarekodi video kuelezea umuhimu wa pweza kwa mzazi  aliyejifungua ili kumsaidia kutoa maziwa. “Watu wa karibu na Wema walivyoona maudhui hayo walitukaribisha nyumbani kwa Wema.

“Tulimpelekea pweza na samaki, tukarekodi video na Wema matokeo yake yakawa makubwa,” anasema.

Ahmed anabainisha kwamba ndani ya siku chache ukurasa wa muuza samaki uliongeza wafuasi kutoka 17 hadi zaidi ya 200,000.

Matokeo hayo yamekuja kuonekana haraka kwani leo kijana huyo hapokei wateja barabarani tu, bali anasafirisha samaki kuanzia Dodoma, Njombe, Morogoro hadi Tanga.


ANAVYOFANYA KAZI

Wengi wanadhani Mwonjaji wa Taifa ana timu kubwa ya wapigapicha nyuma yake, lakini ukweli ni kwamba anafanya kila kitu mwenyewe.

Anasema kitaaluma ni mtaalamu wa habari akiwa na shahada ya uzamili ya mawasiliano.

Anasema anafahamu vyema jinsi ya kuwasiliana na umma kwa kutumia lugha nyepesi na ya kuburudisha ili kuondoa msongo wa mawazo kwa jamii.

Zaidi ya hayo, yeye ni mpigapicha na rubani wa kurusha ndege nyuki (drone), mwenye kampuni ya kupiga picha za harusi.

Katika video zake zote hatumii mpigapichayeyote, bali hujirekodi mwenyewe kwa kutumia kamera ndogo na kipaza sauti chake.

Na ndani ya begi lake la kazi kumejaa vifaa vinavyomfanya aweze kufanya kazi kwa uhuru na ubunifu mkubwa popote anapokwenda.


MILANGO YAFUNGUKA ZAIDI

Kazi ya kuonja imemfungulia milango mikubwa Ahmed, ambapo hivi karibuni alipata ubalozi kutoka katika mgahawa mmoja jijini Dar es Salaam.

Kutokana na ushawishi wake, mgahawa huo umeanzisha mlo maalumu unaofahamika kama “Mwonjaji wa Taifa”.

Licha ya kufurahia kazi yake, Mwonjaji wa Taifa anataja kile anachodai kwamba ni changamoto mbili kubwa zinazomkabili kila siku ambazo ni “kushiba na afya”.

Anasema wakati mwingine anakuwa na ratiba ya kuonja katika maeneo mawili kwa siku, na changamoto inakuja pale anaposhiba mapema, lakini kazi inabidi iendelee.

Pia, kutokana na kula vyakula vyenye mafuta mengi kila siku, hujikuta mwili na umbo likiongezeka.

Hivi karibuni amepanga kuanza kufanya mazoezi  gym ili kujiweka fiti kimwili kwa sababu suala la afya inabidi liendane na mazoezi.

Mwonjaji anatoa ushauri kwa mashabiki wake na vijana wanaotaka kufanikiwa akisema: “Tuendelee kuwa watu halisi, tusifeki maisha.”

Katika hilo, Ahmed anasistiza kuwa uhalisia wa kuishi maisha ya kawaida ndio siri kubwa ya mafanikio na ndiyo maana watu wanamwelewa kwa sababu anayeonekana mitandaoni ndiye wanayekutana naye mtaani.