Yanga kumpiga bei Tshishimbi

Tuesday November 14 2017

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam. Ni ngumu kuamini, lakini ndiyo hali ya halisi baada ya  uongozi wa Yanga umesema upo tayari kuuza kiungo wake Papy Tshishimbi ingawa bado anamkataba wake wa miaka miwili.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kamati ya usajili wa Yanga zinasema kwamba mchezaji huyo anatakiwa nchini Afrika Kusini, Misri na Sweden.

 Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundowns za Afrika Kusini zinajipanga kuleta rasmi ofa mezani kwa Yanga pamoja na timu nyingine kutoka Misri ingawa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alikiri hakuna hata moja ambayo imeshakuja mezani hata wao wanasikia tu kutoka kwa wadau mbalimbali wa Jangwani ila amesisitiza utaratibu ufuatwe.

“Maombi yapo lakini katika hizo timu kutoka Misri na kwingineko hawajaleta barua kwamba kweli wanahitaji kumsajili Tshishimbi, lakini kama wakileta tutakaa nao chini na kuzungumza nao juu ya hilo,” alisema Mkwasa.

“Tshishimbi yupo katika mkataba na Yanga kama kuna timu yoyote kutoka hapa Tanzania au nje inamuhitaji kweli ilete barua ya maombi na sisi tutawambia pesa yetu ambayo tunahitaji ili kumsajili kiuwalali,” alisema Mkwasa bila kuweka rasmi makadirio ya dau wanalomuuza kwa madai kwamba mpaka iwe rasmi.

Mchezaji huyo amekuwa miongoni mwa vipenzi vya mashabiki kutokana na kiwango cha juu alichoonyesha hususani kwenye mechi mbili zilizopita za Simba na Yanga na michezo mingine ya ligi.

Dirisha la usajili linafunguliwa kesho Jumatano na litafungwa Desemba 15.