Njooni sasa tuwanyooshe

Muktasari:

  • Imebainika kuwa kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake, Hussein Nyika imepewa jukumu jipya la kuhakikisha timu inafanya vema katika kila mechi iwe ya Ligi Kuu Bara, Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi ama ile ya Afrika, ambapo mwakani kwa mara nyingine Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

YANGA imefunga usajili kwa kuwanasa wachezaji wawili tu, lakini Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo imetangaza mikakati yake ikitamba kuwa, yeyote atakayejipendekeza mbele yao iwe Simba ama Waarabu, lazima wanyooshwe tu.

Imebainika kuwa kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake, Hussein Nyika imepewa jukumu jipya la kuhakikisha timu inafanya vema katika kila mechi iwe ya Ligi Kuu Bara, Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi ama ile ya Afrika, ambapo mwakani kwa mara nyingine Yanga itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nyika ambaye mapema wiki hii alipewa jukumu la kuongoza kamati hiyo, mbali na kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, alisema anajua jukumu alilopewa ni zito ila kwa wajumbe alionao haoni sababu ya Yanga kushindwa kutetea taji lao la ubingwa wa Bara msimu huu.

Nyika alisema hata kabla hajapewa jukumu hilo, alikuwa katika kamati hiyo kama mjumbe ambapo suala la kutetea taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu Bara ni kitu kisichoepukika na watafanya kweli licha ya Simba kuongoza msimamo kwa sasa.

Alisema, mbali na kupiga hesabu kali za kuona Yanga wanatetea taji lao, lakini pia mikakati yao mingine ni kurejesha taji la FA waliotemeshwa katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Mbao FC na kujipanga kwa mechi ya Ligi ya Mabingwa.

“Kwa namna tulivyojipanga yeyote akija mbele yetu, lazima tumnyooshe kwa sababu tumepania kuwafunga mdomo wote wanaosema vibaya dhidi yetu, iwe ni Simba ama Waarabu tutakaojileta kwenye angaza zetu Afrika,” alisema.

Nyika alisema jambo ambalo wamekubaliana na Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia George Lwandamina ni kuhakikisha katika mechi nne za awali za Ligi ya Mabingwa (yaani za raundi ya awali na kwanza) wanashinda ili watinge hatua ya makundi.

“Ninaposema tunautaka ubingwa kauli hiyo inakwenda na mikakati mizito ambayo kamati tulishaiweka tunajua sasa ndio ligi inaongozwa na Simba, lakini haijaisha kwani, tofauti ya pointi ni mbili. Wanayanga watupe nafasi tufanye kazi.

“Tunajua pia mipango yetu hatuangalii ligi tu tunataka mashindano mengine yote tuwe na ushiriki bora nimeona watu wanatubeza, eti hatutakuwa na jipya katika Ligi ya Mabingwa. Wasubiri waone kwani safari hii tunakuja kivingine.

“Tuna kocha bora na kikosi kizuri chenye muunganiko wa wachezaji wenye uzoefu wa kutosha, endapo Mungu atatusaidia kwa kila mchezaji kuwa na afya bora hakuna timu inayotupa wasiwasi katika ratiba ambayo tumeiona,” alisema Nyika na kuongeza kwa kujiamini;

“Hakuna kinachoshindikana katika kupata ushindi japo tunawaheshimu wapinzani wetu, ila kamati yangu haitaogopa timu yoyote tumeshawafunga Waarabu hivi karibuni tu, hivyo hatuna sababu ya kuhofia kukutana na yeyote Afrika.”

Yanga imepangwa kuanza mechi zake za awali dhidi ya St Louis ya Shelisheli kati ya Februari 9-18 na kama itafuzu katika raundi ya kwanza basi huenda ikakutana ama na El Merreikh ya Sudan au Township Rollers ya Botswana.

Katika Ligi Kuu Bara itakayoendelea tena mwishoni mwa mwezi huu, Yanga itaifuata Mbao kule Mwanza Desemba 31, siku mbili tangu wavaane na JKU katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, lakini kabla ya hapo itakuwa jijini Dar es Salaam kucheza na timu ya Daraja la Tatu, Reha FC katika Kombe la FA.