Mkomola ajivunia uzoefu Yanga
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo amejiunga na Yanga msimu huu baada ya kupata mafanikio katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana akiwa na kikosi cha Serengeti Boys
Dar es Salaam. Mshambuliaji chipukizi wa Yanga, Yohana Mkomola amesema licha ya timu yake kushindwa kutwaa ubingwa anajivunia kupata nafasi ya kucheza pamoja na wachezaji wazoefu.
Mkomola alisema jinsi ambavyo amepiga hatua ya kuongeza ujuzi kwenye soka kama kucheza kwa kujiamini iwe kwenye ligi na michuano ya kimataifa, tofauti na awali ambapo alikuwa anafanya hivyo akiwa na chipukizi wenzake kwenye kikosi cha Serengeti Boys.
"Kuna utofauti mkubwa kucheza watu wenye lika sawa na wale ambao wamekuzidi umri, kwanza hawana papara, wana mbinu nyingi za kumzidi mpinzani, hivyo ndivyo nilivyovipata kwa mastaa wa Yanga.
Kutokana na mambo mengi aliyojifunza msimu huu, Mkomola amesema atatumia muda wake mwingi wa mapumziko kujifua na kujiweka fiti kwa ajili ya msimu mpya, akidai atahitaji kuonyesha uwezo wa juu utakaomfanya asikosekane kwenye kikosi cha kwanza.
"Msimu ulikuwa na changamoto za hapa na pale kwangu, licha ya kwamba nimejifunza mbinu nyingi za kiufundi, nilisumbuliwa na majeruhi ambayo yalifanya nisicheze muda mwingi, lakini kwa sasa napambana ili ligi ikianza nicheze kikosi cha kwanza," anasema Mkomola.
Amemtaja beki Kelvin Yondan kuwa ni kati ya watu waliokuwa karibu nao kwa ushauri wa kujituma na kuangalia mbele kuliko kulewa sifa za mashabiki.
"Yondan ana ushauri wa hekima, mara nyingi alikuwa ananisihi niangalie zaidi kazi kuliko kulewa sifa za mashabiki akisema zinaweza kunifanya nisifike mbali," anasema mshambuliaji huyo.