Dante kashtukia mchezo bwana

Muktasari:

Iko hivi, Dante amemaliza mkataba wake klabuni humo na alishakaa mezani na viongozi wa klabu hiyo na kukubaliana mambo mbalimbali ili asaini mkataba mpya, lakini hajatekelezewa jambo ambalo limempa hofu kwamba dirisha la usajili litafungwa huku akikosa timu ya kucheza msimu ujao.

ZIKIWA zimebaki siku sita tu kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa Ligi Kuu Bara, machale yamemcheza beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ na kutaka kufanya maamuzi ya haraka ili kuhakikisha anaendelea kubaki ligi hiyo.

Iko hivi, Dante amemaliza mkataba wake klabuni humo na alishakaa mezani na viongozi wa klabu hiyo na kukubaliana mambo mbalimbali ili asaini mkataba mpya, lakini hajatekelezewa jambo ambalo limempa hofu kwamba dirisha la usajili litafungwa huku akikosa timu ya kucheza msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dante, alisema siku za dirisha la usajili kufungwa zimebaki chache na kwa ukimya uliopo anaona kabisa anatakiwa kufanya maamuzi mengine kwani bado anataka kuendelea kuwepo ligi kuu.

“Dirisha linakaribia kufungwa na timu nyingi zinakamilisha usajili wao, bado sijasaini licha ya kuzungumza nao, lakini ukimya wao ndio unanifanya nifikirie kitu kingine kichwani kwangu, vinginevyo nitakuwa na wakati mgumu katika maisha yangu ya soka,” alisema Dante.

Dante alifunguka sababu kubwa ya yeye kuchelewa kusaini mkataba mpya ni kutokana na kutopatiwa pesa ya usajili.

“Sikupewa pesa ya usajili, nisingeweza kusaini mkataba, ifahamike kwamba kazi yangu ni mpira na ndio kitu ambacho kinafanya maisha yangu yaende, hivyo pesa ndio itakayonifanya nibaki au lolote linaweza kutokea,” alisema.