JICHO LA MWEWE: Tatizo la Yanga ni Mahadhi sio Simon Msuva

Muktasari:

Hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani, inategemea tu ni kiasi gani cha fedha kinachotakiwa.

YANGA inafunga mabao machache kuliko wakati mwingine wowote katika miaka ya karibuni. Ina mabao manne tu, ni mabao mawili pungufu kwa mabao ambayo Emmanuel Okwi amefunga peke yake ndani ya mechi mbili tu. Nyakati zinageuka.

Maneno ya chini chini yanasemwa jinsi ambavyo Yanga wanamkosa sana Simon Msuva. Ni kweli. Niliwahi kuandika mahala mitandaoni mchezaji ambaye Yanga itamkosa zaidi ni Simon Msuva kuliko Haruna Niyonzima.

Hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani, inategemea tu ni kiasi gani cha fedha kinachotakiwa. Wamorocco walifika bei na Yanga ikauza. Hakuna kosa hapo. Aliuzwa Cristiano Ronaldo, aliuzwa Neymar, aliuzwa Diego Maradona, nini Msuva?

Arsenal ilipomuuza Nicolas Anelka kwenda Real Madrid kwa Pauni 22 milioni mwaka 1999 iliweza kujenga uwanja wake wa mazoezi London Colney na pia pesa iliyobaki ilimnunua Thierry Henry.

Tatizo la Yanga nalipeleka binafsi kwa kijana anayeitwa, Juma Mahadhi. Alipoondoka Msuva ilibidi Mahadhi azibe pengo kwa urahisi tu. Lakini naambiwa Mahadhi ana mambo mengi nje ya uwanja. Sina uhakika. Sijui. Ninachojua, hajajitendea haki mwenyewe wala klabu yake.

Kabla ya Msuva Yanga alikuwepo Mrisho Ngassa. Ndiye ambaye alikuwa anaipeleka Yanga mbele kwa kasi zaidi. Ndiye aliyekuwa anapika mabao mengi ya akina Boniface Ambani na washambuliaji wengine wa Yanga. Pia ndiye aliyekuwa anafunga mabao mengi.

Jeuri kubwa ya Yanga kuachana na Ngassa baadaye ilitokana na kuibuka kwa Msuva. Staili yao ya soka ilifanana kutokana na kasi kubwa ya Msuva. Msuva alionekana kijana zaidi. Yanga walikuwa katika mikono salama.

Baada ya Msuva mchezaji ambaye alionekana angepeleka mwendelezo wa Ngassa, kisha Msuva mwenyewe ni Mahadhi. Tatizo la vijana wa siku hizi wanachezea nafasi wanazopata katika timu kubwa, lakini zaidi ni kwamba wanachezea vipaji vyao.

Mahadhi niliyemwona katika mechi ya kwanza akiwa na jezi ya Yanga alikuwa ana kasi, akili, nguvu na uwezo wa kupiga mashuti angali anakimbia. Nilidhani alikuwa tishio zaidi kwa nafasi ya Msuva kwa sababu alionekana kuwa ana kipaji zaidi ya Msuva.

 Bahati mbaya kwa sasa haonekani hivyo. Anaonekana mchezaji wa kawaida. Tatizo la vijana wa siku hizi hawana njaa. Hawana kiu. Hawapanii mechi wala hawapanii kuzivaa jezi za Simba na Yanga kwa muda mrefu. Jezi hizi wanazipata kiurahisi sana tofauti na ilivyokuwa awali.

Kuna mambo mawili ambayo Mahadhi amejiangusha kutokana na kipaji chake. Kwanza kabisa kabla hata ya Msuva kuondoka alipaswa kumweka staa huyu wa timu ya taifa katika mazingira magumu ya nafasi yake. Hilo halikutokea. Msuva aliendelea kuwa staa na aliendelea kuwa mfungaji bora klabuni.

Pili, kama hilo halikutokea, basi alipaswa moja kwa moja kuwa mbadala wa Msuva bila ya viongozi kuulizana. Hili nalo halijatokea. Hapo ndipo unapojaribu kujiaminisha kuna kitu kinamsumbua Mahadhi ndani na nje ya uwanja.

Pia kinadhihirisha jinsi ambavyo siku hizi soka la ushindani limeondoka nchini. Kuna picha ya zamani ya timu ya taifa huwa inatembea mitandaoni. Hiyo picha ina Zamoyoni Mogella, Hamis Gaga, Hussein Marsha na Athuman China.

Unaweza kuachana na Mogella ambaye alikuwa ni mshambuliaji, unajaribu kujiuliza kuhusu hawa watu watatu, Gaga, China na Marsha. Unajiuliza jinsi ambavyo kocha alikuwa na wakati mgumu katika kupanga kikosi chake. Ni nani alianza nani alikaa benchi?

Zaidi ya kujiuliza swali hilo unajiuliza pia jinsi ambavyo kulikuwa na wachezaji wengine wa nafasi ya kiungo ambao walikuwa mahiri katika zama hizo. Dadi Athuman, Ally Maumba, Idrisa Ngulungu na wengineo. Nafasi zao zilikuwa wapi kikosini hapo?

Katika kizazi cha leo, ukiletewa picha ya vikosi vya sasa miaka mingi baadaye utajua tu Msuva alikuwa anaanza kila siku mbele ya Mahadhi. Utajua tu kulikuwa hakuna mtu wa kumuweka benchi Kamusoko. Utajua tu maisha yalikuwa rahisi kwa Donald Ngoma. Hiki ndicho ambacho wachezaji wa kisasa akina Mahadhi wanatuandalia.

Kama angekuwa mchezaji makini anayejitambua na kupigana, nafasi ya Msuva ingekuwa yake. Si tu katika jezi ya Yanga bali hata katika jezi ya timu ya taifa. Na hata safari ya Morocco ingeweza kuwa yake.