Zahera amegoma kuondoka Yanga

Muktasari:

  • Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema licha ya uongozi kupokea simu kutoka Zambia ikiwa inahitaji kumchukua, hawezi kukubali hata ikija ofa kubwa namna gani.
  • "Nilijiunga na Yanga niliikuta ikiwa katika hari mbaya kiuchumi nitaendelea kuwafundisha kwasababu niliingia mkataba wa makubaliano wakiwa hawana fedha sina sababu ya kuwakimbia,"


KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amethibitisha kutia nanga ndani ya kikosi hicho kwa kauli yake kwamba hata angepewa dola 40,000 hawezi kuondoka.

Hayo ameyasema siku chache baada ya uongozi wa Yanga kuthibitisha kupokea simu kutoka moja ya timu ya Ligi Kuu Zambia wakiomba mazungumzo kuhusu kuwauzia kocha huyo ambaye ana mkataba wa miaka miwili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera ambaye tayari ametimka nchini na kwenda kujiunga na timu ya Taifa ya Congo akiwa kama Kocha Msaidizi alisema hawezi kuiacha Yanga hata ikiwa katika hari mbaya vipi, kwani yeye haamini kama maisha ni pesa pekee bila utu.

“Mimi kama mwalimu nimekuwa nikiwasisitiza wachezaji wangu kila siku kuhakikisha wanavumilia hali wanayokumbana nayo sasa katika klabu yao, nawaambia wapambane kuibeba timu naanzia wapi kuwaakimbia naondoka kisa maslahi,”

“Ni kweli nimeambiwa na uongozi kuwa kuna timu kutoka Zambia, mimi sijajua ni timu gani wamewapigia simu kuwaomba niende kuifundisha timu yao kiukweli sipo tayari kuwaacha wachezaji wangu na kuiacha Yanga, nitaondoka nikifukuzwa au Yanga ikifa,” alisema.

Zahera aliongeza kuwa ameikuta timu hiyo ikiwa vibaya kiuchumi na aliweza kukubaliana na hali hiyo kwa kuingia mkataba wa miaka miwili, hivyo hawezi kuikimbia kwa sababu hata akitoka Yanga na kwenda Zambia huenda akakutana na changamoto kama hiyo.

“Hao viongozi kutoka Zambia wanaweza wakanitafuta sasa wakiwa na uwezo mzuri wa fedha na baadaye wakakosa hiyo fedha nitakimbilia wapi tena, nitaendelea kubaki Yanga kwa hali yoyote sina tabia ya kuangalia maslahi zaidi huwa na utu ni muhimu kwangu,” alisema.

Zahera alijiunga Yanga akiziba nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, George Lwandamina ambaye aliikimbia klabu hiyo kutokana na ukata uliowakumba na kuamua kurudi katika timu yake ya zamani ya Zesco ambayo ndio anaitumikia hadi hivi sasa.