Yanga bila Manqoba, Dodoma Jiji, JKT Tanzania kazi ipo
Muktasari:
- Kukosa matokeo ya ushindi katika michezo miwili iliyopita ya Ligi Kuu Bara, ikifungwa mabao 2-1 dhidi ya Simba na ikitoka suluhu dhidi ya TRA United, ndiyo sababu ambayo inaifanya Yanga leo kuhitaji ushindi.
YANGA inashuka dimbani leo bila ya uwepo wa Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi aliyesitishiwa mkataba wake, huku jukumu lililopo kwa benchi la ufundi chini ya Simo Dladla anayekaimu nafasi hiyo, ni kutaka kurejesha tabasamu kwa mashabiki wake kupitia mechi hiyo dhidi ya Mashujaa FC.
Kukosa matokeo ya ushindi katika michezo miwili iliyopita ya Ligi Kuu Bara, ikifungwa mabao 2-1 dhidi ya Simba na ikitoka suluhu dhidi ya TRA United, ndiyo sababu ambayo inaifanya Yanga leo kuhitaji ushindi.
Kama Yanga itashinda leo, itaendelea kusalia nafasi ya pili ikifikisha pointi 22, kwani sasa inazo 19 katika mechi nane ilizocheza, ikishinda sita, imepoteza moja sawa na suluhu iliyopata.
Kwa upande wa Mashujaa katika mechi nane ilizocheza imeshinda nne, imefungwa nne, ipo nafasi ya nane na inamiliki pointi 12, ikitokea imeshinda itafikisha alama 15.
Licha ya kocha Dladla kutambua ugumu utakaokuwepo katika mechi hiyo, amesema amewajenga wachezaji kiakili ili kusahau matokeo ya mechi zilizopita, bali ni nafasi kwao kuhakikisha mashabiki wanarejesha tabasamu usoni.
“Ingawa tuna chalenji za hapa na pale, lakini haiwezi kuturudisha nyuma, badala yake tunahitaji kufokasi na mechi zilizopo mbele yetu,” amesema kocha Dladla.
Kwa upande wa golikipa wa timu hiyo, Aboutwalib Mshery amesema: “Kocha Dladla alikuwepo na kikosi, amepata muda wa kuangalia wapinzani wetu ni wa aina gani, ndiyo maana ametuandaa kulingana na ushindani ambao tunakwenda kukabiliana nao, kama wachezaji tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili tuendelee kupambana kwa pamoja.”
Wakati Kocha wa Mashujaa FC, Amani Josiah amesema anatambua wanakwenda kukutana na bingwa mtetezi kwa mara nne mfululizo, hivyo matokeo iliyopata Yanga dhidi ya Simba na TRA United, hayawezi kuzuia ushindani na ugumu wa mechi.
“Yanga ni timu ya daraja la juu, ina makocha wenye mbinu nzuri, wachezaji wa madaraja ya juu, itakuwa mechi bora na ushindani, kwa upande wetu tumejiandaa naamini wachezaji watakuwa na chalenji nzuri dhidi yao,” amesema Josiah.
Kwa upande wa beki wa timu hiyo, Baraka Mtuwi, amesema: “Makocha wameishatuandaa kwa mbinu, kikubwa tunawaomba mashabiki wa Mashujaa kujitokeza kwa wingi kuja kutupa sapoti.”
Msimu uliopita mechi iliyopigwa Januari 19, 2026, Yanga ilishinda kwa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa, kisha Juni 13, 2026 bado Wanajangwani waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wanamapigo na Mwendo.
Mechi nyingine leo itakuwa kati ya Dodoma Jiji dhidi ya JKT Tanzania ambayo msimu uliopita haikuambulia pointi hata moja.
Ambapo Januari 30, 2026 JKT Tanzania ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Dodoma, kisha Juni 24, 2026 zilitoka suluhu, pamoja na matokeo hayo kocha wa Dodoma Jiji, Vincent Mashami amesema: “Tunakutana na JKT Tanzania ambayo ina kocha mwenye mbinu, siwezi kutabiri matokeo ila tutapambana kupata alama tatu.”
Kwa upande wa kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema: “Chelenji ya ushindani tunaitarajia, Dodoma siyo timu ya kuibeza ina wachezaji wazuri na kocha mwenye mbinu nzuri, tumejipanga dakika 90 zitaamua nani atatoka na pointi tatu.”