Winga mpya Yanga huyu

Muktasari:

  • Kocha wa Yanga, Zahera anataka kusajili winga mmoja kwa lengo la kuongeza kasi katika safu yake ya ushambuliaji

DIRISHA dogo la usajili linafunguliwa Novemba 15, ni wazi kwamba kila timu sasa inahaha kuhakikisha inaziba mapengo ambayo yamejitokeza katika Ligi Kuu inayoendelea. Yanga nayo haichezi mbali, inasaka wakali ambao wanaweza kuwapaisha na kutikisa katika ligi ikiwa ni pamoja na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Yanga waliibuka na straika Heritier Makambo katika dirisha la usajili lililopita, lakini wamegundua kwamba mchezaji huyo hajafikia kiwango thabiti walichokuwa wakikihitaji na sasa wameamua kumtafuta winga wa kumlisha raia huyo wa DR Congo.

Wanajagwani hao wamefanikiwa kumshawishi winga Ruben Bomba raia wa DR Congo (klabu imehifadhiwa), ambaye tayari ameshakubali kutua katika klabu hiyo.

Juzi kati Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera aliweka wazi kwamba anataka kuletewa winga mmoja matata atakayekuwa na kazi ya kuwalisha washambuliaji, ni wazi karibia azma yake itatimia.

Pia juzi Jumapili mara baada ya mechi dhidi ya Ndanda ambayo walitoka sare ya 1-1, kocha Zahera aliliambia Mwanaspoti kuwa kupungua makali kwa Makambo kunatokana na kutolishwa ipasavyo huku wachezaji wa wake wa pembeni wakishindwa kuwa na muendelezo mzuri wa viwango vyao.

Zahera alisema nyota wake wake wawili Deus Kaseke na mkongwe Mrisho Ngassa bado hawajaweza kufanya anachokitaka na kuwa ndiyo maana ametaka kusajiliwa kwa mtu muafaka angalau mmoja kutoka katika eneo hilo.

“Kaseke kwa kiwango cha juu sana kwasasa lakini Makambo naye amekuwa akikosa mabao kirahisi huku wakati mwingine hapewi mipira sahihi,”alisema Zahera.

“Ndiyo maana nataka mtu wa kuongeza nguvu tunayoitaka katika safu yetu ya ushambuliaji, ngoja tuone kipi tutafanya muda wa kusajili ukifika.”

Bomba, ndiye chaguo la kwanza la Zahera na tayari mabosi wa usajili chini ya Mwenyekiti Hussein Nyika walishaanza kazi ya kuhakikisha anatua nchini.

Taarifa kutoka ndani ya kamati inasema kwamba Bomba ameshakubali kutua Yanga ambapo raia huyo wa DR Congo anataka kuungana na Zahera ambaye pia ni Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya DR Congo.

“Tumeshafanya naye mazungumzo kilichokuwa kinahitajika ni utulivu ndani ya klabu yetu,”alisema bosi huyo. “Huyu Bomba (Ruben) ni winga mzuri, tumeona kasi yake uwanjani. Akifika hapa mashabiki watakubali ninayosema.”