Wakili Kuuli ajiuzulu uwenyekiti kamati uchaguzi TFF

Muktasari:

Wakili Kuuli anapozungumza huwa nazungumza kwa niaba ya kamati ya uchaguzi na hata nilipozungumzia suala la uchaguzi wa Simba ilikuwa ni uamuzi wa kamati, mtu mwingine nje ya kamati hawezi kunipinga.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Revocatus Kuuli amejiuzulu kuongoza kamati na uongozi wa shirikisho hilo umesema kujiuzulu kwake siyo tatizo kwao kazi zitaendelea kama kawaida.

Kuuli amejiuzulu nafasi hiyo ikiwa ni siku chake tu tangu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau amwandikie barua ya kujieleza ndani ya siku tatu akieleza kwa nini amesimamisha uchaguzi wa Simba.

Hata hivyo katika taarifa ya Kuuli alisema tarehe ya uchaguzi ya Simba itabaki ile ile iliyopangwa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba ila wafanye marekebisho baadhi ya kanuni ambazo zipo kinyume na kanuni za uchaguzi za TFF.

Kuuli yeye ameweka wazi kuwa hawezi kuendelea kuongoza Kamati hiyo kwa kile alichodai ni kuwepo na ubabaishaji na kuingiliwa na majukumu ya Kamati wakati yeye anasimamia sheria.

Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani alizungumzia kujiuzulu kwa Kuuli kwamba hakutapunguza wala kuongeza jambo lolote ndani ya TFF.

"Amejiuzulu Kuuli na siyo kamati nzima, kuna makamu wake ambaye ataendelea na majukumu hayo ya kusimamia chaguzi zilizopo na kazi zingine za Kamati, hivyo hakuna tatizo lolote na kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa," alisema Nyamlani.

Hivi sasa klabu ya Simba ipo katika mchakato wa uchaguzi utakaofanyika Novemba 4 na wamefikia hatua ya kukata rufaa baada ya kupitia pingamizi ambapo rufaa hizo hukatwa kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi na TFF iliyopo ndani ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Bodi ya Ligi nayo inafanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya Mwenyekiti iliyoachwa wazi na Clement Sanga aliyejiuzulu na wasimamizi ni kamati hiyo, lakini tangu kuchukuwa na kurudishwa fomu lifungwe Septemba 25 hakuna kinachoendelea.