Usajili wa Obrey Chirwa uko hivi!

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo Mzambia msimu uliopita alifunga mabao 12, kabla ya kutimkia Misri baada ya kushindwana na viongozi wa Yanga kuhusu malipo ya mshahara wake

MABOSI wa Yanga hawataki kupoteza muda na tayari wamemleta straika wao wa zamani, Obrey Chirwa ambaye amekuja kusikilizia dili la kutua kwa mara nyingine klabuni hapo, lakini ghafla mgawanyiko wa chini kwa chini umeanza.

Mashabiki, wachezaji na baadhi ya viongozi wa Yanga wanataka kuona dili la straika huyo kuvaa jezi za njano na kijani likitiki fasta, lakini wengine hawaoni sababu ya dili la usajili huo kutokea kwa sasa.

Iko hivi, Chirwa ambaye aliondoka Yanga na kutua nchini Misri baada ya kumaliza mkataba wake, inadaiwa amevunja mkataba na klabu yake ya huko kutokana na kushindwa kumlipa stahiki zake walizokubaliana wakati anasaini mkataba huko.

Kutokana na hali hiyo Yanga ambayo inatafuta straika ili kunogesha safu yake inayobebwa na Herieter Makambo na Ibrahim Ajibu, ikamuita nchini ili kujadiliana naye juu ya kurejea klabu hiyo.

Chirwa mwenyewe ndiye aliyeomba kurejea Yanga na Mwanaspoti kama kawaida likatangaza mchakato mzima ulivyokuwa hivyo, mabosi wa Yanga wakamvuta nchini kumsikiliza.

Katika majadiliano hayo hata kabla ya Chirwa hajafika katika maongezi ya mkataba huo mvutano mkubwa ukaibuka.

Msimamo wa Zahera

Kocha Mwinyi Zahera ameliambia Mwanaspoti kuwa hana tatizo na kipaji cha mshambuliaji huyo, lakini shida ni nidhamu yake.

Zahera alisema tabia aliyoonyesha Chirwa kabla ya kutimka kwa kuigomea Yanga kucheza mechi nne kufuatia kuidai klabu hiyo ni kitu ambacho kilimkasirisha sana.

“Chirwa sio mchezaji mbaya, lakini sidhani kama anahitajika hapa alitugomea wakati nafika hapa alikataa kucheza mechi nne akisema anataka alipwe,” alisema Zahera.

“Tulimuhitaji wakati tunakwenda Algeria akagoma, lakini pia aligoma kwenda Shinyanga na Mbeya tukafungwa sidhani kama anatufaa kwa sasa.”

Azam wawatibulia Yanga

Wakati Zahera akimkataa Chirwa kumbe mabosi wa Yanga kumleta Chirwa nchini ni kama waliiwahi Azam ambao, walichelewa kidogo kumtumia tiketi ya kumleta nchini.

Azam ilitangulia kufanya maongezi na Chirwa na walichotaka ni kuja asimame na Mzimbabwe Donald Ngoma katika safu yao ya ushambuliaji.

Mabosi wa Yanga hawana tatizo na maamuzi ya Zahera, lakini kinachowatisha ni kumpeleka Chirwa Azam ambako kama ataungana na Ngoma kisha wakaelewana balaa linaweza kutokea.

Hata hivyo, mpaka tunakwenda mitamboni bado majadiliano yalikuwa yakiendelea na lolote linaweza kutokea kuhusiana na dili hilo huku hamu kubwa ya mashabiki ni kumuona Chirwa.