Sifa tano viongozi wapya Yanga zaanikwa

Muktasari:

  • Wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea, Mwaisabula alisema Yanga ya sasa si ile ya miaka 50 iliyopita, hivi sasa inahitaji kiongozi mwenye upeo mkubwa katika kuongoza.

WAKATI wanachama wa klabu ya Yanga wakisalia na siku 10 kupata uongozi mpya, aliyewahi kuwa kocha wa timu hiyo, Kenny Mwaisabula ametaja sifa tano za mtu anayestahili kuongoza klabu hiyo.

Yanga itafanya uchaguzi Mei 5 jijini Dar es Salaam kujaza nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya utendaji ambao walijiuzuru kwa nyakati tofauti.

Wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea, Mwaisabula alisema Yanga ya sasa si ile ya miaka 50 iliyopita, hivi sasa inahitaji kiongozi mwenye upeo mkubwa katika kuongoza.

“Bahati nzuri wagombea wengi wana elimu ya kutosha, katika hilo hakuna mjadara, lakini wanapaswa mbali na taaluma yao wawe na sifa zingine za ziada,” alisema Mwaisabula na kuzitaja sifa nyingine kuwa ni kiongozi atakayepewa ridhaa hiyo lazima awe mbobezi katika masuala ya michezo.

“Anapaswa kuijua kwa undani Yanga, ajue inahitaji kitu gani kwa sasa sio achaguliwe kwa kuwa ana porojo, Yanga ya leo sio ya Jana,” alisema.

Alisema pia kiongozi atakayepewa ridhaa awe na uwezo wa kutengeneza mikakati ya kuipeleka Yanga kule ambako kila Mdau anahitaji kuona klabu hiyo kongwe ya soka inafika.

“Wasichague viongozi kwa papara, mihemko na makundi, kila mmoja afanye uamuzi kwa maslahi ya klabu yao kwa kuchagua viongozi wenye tija na klabu.

“Kwani wanachama wakimchagua mtu mwenye sifa hizo, hakuna shaka kuwa watu wa maana wenye fedha zao watajitokeza kuwekeza, Yanga itatengeneza mfumo wa kujitegemea, kuwa na miradi yake kama kuuza jezi na vifaa hata kuuza wachezaji,” alisema Mwaisabula ambaye ni mkereketwa wa Yanga.