Mnata: Yanga inabadili maisha yangu
Muktasari:
Kipa wa Yanga, Metacha Mnata amesema anautazama msimu huu kama wakumtambulisha zaidi mbele ya wadau wa soka nchini, kutokana na timu aliopo kuwa kubwa hivyo anaamini atafanya kazi ya kuisaidia klabu kutimiza malengo waliojiwekea.
Dar es Salaam. Kipa wa Yanga na Taifa Stars, Metacha Mnata amesema licha ya kucheza muda mchache ndani ya kikosi cha Wanajangwani ameanza kunufaika kimaisha tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Mnata alisema licha ya changamoto ya presha iliopo Yanga kinachohitaji matokeo mazuri katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufungwa na Ruvu Shooting, kutoka sare ya mabao 3-3 na Polisi Tanzania na kushinda dhidi ya Coastal Union, amekiri kuonja matunda.
"Hii ni mara ya kwanza kwangu kucheza Yanga ni klabu kubwa, ina presha tofauti na timu nilizopitia kwa maana ya Azam FC na Mbao FC ambako mchezaji huwezi kuwa katika mawazo makubwa kama huku, lakini nimeanza kunufaika,"
"Kupitia kujulikana najikuta baadhi ya mambo yangu ya kimaisha yanakwenda, hilo ni jambo linaloendelea kunipa moyo wa kupambana kuamini siku moja nitakuwa mtu wa tofauti katika soka la Tanzania," alisema Mnata.
Kipa huyo anautazama msimu huu kuwa na ushindani wa hali ya juu utakaomfanya kiwango chake kiwe bora.
"Ugumu wa kazi ndio unaomtambulisha mtu kuwa bora, naendelea kujituma na kujifunza kwa wale ambao wamenitangulia kwa uzoefu, naamini utakuwa mzuri kwa upande wangu kutoka hatua moja kwenda nyingine," alisema Mnata.