Metacha: Nilimsoma mpigaji wa penalti ya Township Rollers
Muktasari:
Mnata baada ya wapinzani wao Township Rollers kupata penalti hakuwa na wasiwasi aliwatuliza wachezaji wenzake na kumsubiri mpigaji
Dar es Salaam. Kipa wa Yanga, Metacha Mnata amesema kupangua penalti kwake haikuwa ya kubahatisha kwani alimsoma vyema mpigaji.
Mnata amesema baada ya wapinzani wao Township Rollers kupata penalti hakuwa na wasiwasi aliwatuliza wachezaji wenzake na kumsubiri mpigaji.
Wakati kiungo Segolame Boy akijiandaa kupiga penalti hiyo Mnata amesema alijua mpigaji huyo alitaka kumdanganya wapi anapopeleka mpira kwa kutumia macho yake na baadaye kuidaka kiurahisi.
Alisema alitambua umuhimu wa kuwa mtulivu na kucheza penalti hiyo kwa kuwa kama wapinzani wao wangefunga ingewaongezea nguvu huku wao wakiingia katika presha ya kupoteza.
Kipa huyo alisema licha ya ushindi wao huo mchezo huo haukuwa rahisi kwani walihitaji kupambana zaidi kuhakikisha wanaitetea klabu yao na mwisho wa mchezo walifanikiwa.
Aidha Mnata alisema kuelekea mchezo dhidi ya Zesco ya Zambia wanatambua kwamba haitakuwa mechi rahisi na kwamba watajipanga kuhakikisha wanashinda vizuri.