Makambo, Amiss Tambwe kila mmoja ana jukumu lake

Muktasari:

  • Mwandila aliongeza kuwa anapambana kuwaweka sawa viungo wake kuelekea mchezo huo kutokana na kuonyesha mapungufu mchezo wao wa mwisho ugenini na kwamba ubora wa wapinzani wao unampa mtihani mgumu.

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila amewafungia kazi Heritier Makambo, Amis Tambwe na Mrisho Ngassa na kuweka wazi kuwa kama watafanyia kazi maelekezo yake basi mchezo wao na Alliance hawatakuwa na kazi ngumu ya kufanya.

Yanga inatarajia kushuka dimbani Machi 30, mwaka huu, kumenyana na Alliance mchezo wa robo fainali Kombe la FA utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata matokeo uwanja huo. Mwandila alisema anawafahamu vizuri wapinzani wake kuwa wanacheza mpira wa kasi, wana nguvu hivyo ameamua kukaa na nyota hao kuwapa mbinu za kupata matokeo mazuri yatakayowafanya wasonge mbele.

Alisema ingawa wamekutana nao mara mbili michezo ya Ligi Kuu Bara bado waangalia CD za michezo waliyokutana nao ili kuwasoma zaidi upungufu wao na jinsi ya kuwadhibiti wachezaji wao ambao ni tishio.

“Hatuna cha kupoteza kuelekea mchezo huo tupo makini kila idara tunapambana kuhakikisha tunapata matokeo uwanja wa Kirumba, sio kazi rahisi kwetu kwani tunakutana na wapinzani ambao ni bora kila idara,”

“Wana nguvu, wachezaji vijana na wana kasi tunatarajia kukutana na changamoto kubwa kutoka kwao lakini tumejipanga kukabiliana nazo kwasababu tunatambua umuhimu wa mchezo huo, Ngassa na Makambo wanakasi ya kukimbia na mipira Tambwe atakaa tayari kwaajili ya kumalizia mipira mirefu itakayokuwa inapigwa,” alisema.

Alisema hawawezi kucheza mchezo sawa na wapinzani wao wanatarajia kutumia mbinu mbadala ambayo itawasaidia wao kupata matokeo kama ilivyokuwa michezo iliyopita na kuweka wazi kuwa lengo lao ni kupata matokeo mapema ili kuwatoa mchezoni wapinzani wao.

Mwandila aliongeza kuwa anapambana kuwaweka sawa viungo wake kuelekea mchezo huo kutokana na kuonyesha mapungufu mchezo wao wa mwisho ugenini na kwamba ubora wa wapinzani wao unampa mtihani mgumu.

“Alliance kila idara iko vizuri na inaweza kucheza mpira ya chini sana pasi fupi fupi ili timu yangu iweze kupata matokeo mapema nimeanza na safu ya ushambuliaji na kiungo ambao ni muhimu sana mchezo wetu wa mwisho tulipata matokeo lakini kwa kiasi kikubwa tulionekana kuwa na mapungufu katikati,”

“Umakini wa washambuliaji ndio utakaoamua matokeo katika mchezo huo kwa kiasi kikubwa nimefanya marekebisho maeneo muhimu kwetu,” alisema