Ivo: Kakolanya anajiua

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Ivo aliyewahi kuzidakia timu mbalimbali ikiwemo Yanga, Simba, Azam, Gor Mahia, St George na Taifa Stars, alisema anachokifanya Kakolanya katika soka la sasa hawezi kufika mbali kwani anajipotezea imani.

KIPA Beno Kakolanya amekaa pembeni na timu yake ya Yanga akishinikiza alipwe madai yake ya pesa za usajili na mishahara lakini mkongwe wa soka Ivo Mapunda amemwambia huko ni kujishusha kiwango chake kwa kuweka masilahi mbele.

Ivo amesema ubora wa mchezaji yeyote unatokana na kucheza mara kwa mara ambapo Kakolanya tayari alikuwa kwenye mipango ya Kocha Mwinyi Zahera aliyekuwa akimtumia kama kipa wake namba moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ivo aliyewahi kuzidakia timu mbalimbali ikiwemo Yanga, Simba, Azam, Gor Mahia, St George na Taifa Stars, alisema anachokifanya Kakolanya katika soka la sasa hawezi kufika mbali kwani anajipotezea imani.

“Kakolanya ni kipa mzuri, ila anachokifanya sasa ni kujidanganya maana kiwango chake kinashuka, kukaa nje muda mrefu hakumjengi mchezaji hata kama hana mpango wa kucheza Yanga huko anakokwenda anapoteza uaminifu labda kama anaenda nje pia wanafuatilia hadi mechi ya mwisho pamoja na historia ya mchezaji.

“Miaka michache iliyopita tulikuwa tunaangalia zaidi kupata nafasi ya kucheza ili uonekane na timu zingine, masilahi lilikuwa jambo la pili ila sasa ni tofauti kabisa na wachezaji wetu hawa, masilahi kwanza kucheza baadaye bila kujali wanapeleka wapi viwango vyao, hii inawaumiza wachezaji wengi.

“Kakolanya ni kijana mwenye umri mdogo kukaa nje kunamuumiza yeye na si mtu mwingine, Yanga sasa hivi inafanya vizuri angekuwepo yeye nafasi yake ilikuwa wazi sana ya kucheza lakini Ramadhan Kabwili kakamata dimba na ataendelea kuwa bora zaidi baada ya Klause Kindoki kutoka mchezoni alipofanya vibaya kwenye mechi za nyuma,” alisema Ivo

Kuhusu kasi ya Yanga, Ivo alisema kama kuna timu itawashangaza wengi basi ni Yanga kama wachezaji wataendelea kuwa na ari kama ilivyo sasa.

“Mpaka sasa ligi bado haijasomeka, farasi wanapishana kuchukuwa nafasi, atakayeteleza ni yule atakayeachia pointi, timu ndogo mambo magumu, Simba walifanya usajili mzuri zaidi kuliko Yanga lakini kama wachezaji wa Yanga wakiendelea na ari hii tutarajie kushangazwa mwisho mwa msimu.

“Yanga ina matatizo ya kifedha, haina wachezaji wa kuogopwa sana ila wana ushirikiano, kocha wao anajua kutengeneza saikolojia za wachezaji wake.”