Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk. Msolla: Tunaifumua Yanga

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti Dk Msolla alisema ili kuifanya Yanga kuwa na ushindani wa kweli ni lazima mapinduzi makubwa yafanyike kwenye kikosi hicho. Alisema usajili wa msimu ujao utafanyika kwa umakini mkubwa na kazi ya kwanza itakuwa ni kukifumua kisha kukisuka upya kwa ajili ya kusaka mafanikio ndani na nje.

BOSI mpya wa Yanga, Dk Mshindo Msolla na wasaidizi wake ambao wamechaguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita, walikuwa kwenye jukwaa wakati timu yao ikikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Lipuli FC kwenye nusu fainali ya Kombe la FA.

Kipigo hicho ambacho kilikuwa cha kwanza kwa viongozi hao ambao ndio walitoka kuchaguliwa na wanachama kwenye Mkutano Mkuu, kilikuwa na maumivu makali kwani, ndio kimefuta ndoto za mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, kushiriki kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.

Kwa sasa Yanga imeondolewa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na watani zao Simba, ambao ndio mabingwa watetezi baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru, jana, haina matumaini ya kubeba ubingwa huo. Mlango pekee ambao ungeweza kuwaingiza Yanga kwenye michuano ya kimataifa ni kupitia FA, lakini Lipuli FC ikazima ndoto kwa kuitupa nje ya michuano hiyo na sasa bingwa wake ambaye atashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, ataamuliwa kati ya Lipuli na Azam FC.

Hata hivyo, baada ya kushuhudia chama lake likiondolewa kwa aibu, Dk Msolla akafunguka mazito akisema msimu utakapomalizika tu, basi kikosi kizima cha Yanga kitafumuliwa.

Akizungumza na Mwanaspoti Dk Msolla alisema ili kuifanya Yanga kuwa na ushindani wa kweli ni lazima mapinduzi makubwa yafanyike kwenye kikosi hicho. Alisema usajili wa msimu ujao utafanyika kwa umakini mkubwa na kazi ya kwanza itakuwa ni kukifumua kisha kukisuka upya kwa ajili ya kusaka mafanikio ndani nan je.

“Ndani ya kikosi chetu kuna kazi kubwa ambayo itafanyika, ukweli ni kuwa kwa sasa hatuko kwenye ubora ambao Yanga inatakiwa kuwa nao. Ubora wa kikosi chetu haulingani na uzito wa jina la Yanga,” alisema Dk Msolla, ambaye ameshinda nafasi ya Mwenyekiti akichukua nafasi iliyoachwa na Yusuph Manji kwa kura 2071.

Pia, alifichua kuwa aliwahi kukutana na Kocha Mwinyi Zahera na kufanya mazungumzo ambapo, Mkongomani huyo alimweleza kuwa kwa sasa kuna wachezaji nane ama tisa ndio wako kwenye ubora unaotakiwa.

“Niliwahi kuzungumza na Zahera kabla hata sijachaguliwa kushika nafasi hii na alionyesha kwamba, kuna wachezaji nane au tisa pekee anaridhishwa na viwango vyao na ndio wanastahili kuendelea kuwepo Yanga msimu ujao hivyo, utaona ni kazi kubwa tutakwenda kuifanya hapa ili kuweka mambo sawa,” alisema Dk Msolla.

Pia, Dk Msolla ambaye kitaaluma ni kocha, alisema anafahamu Zahera anahitaji fungu la maana kwa ajili ya kunasa wachezaji wenye viwango vya kimataifa.

Alisema kwenye usajili huo kiasi cha zaidi ya Sh1.5 bilioni zinahitajika na uongozi wake upo tayari kupambana kusaka hata Sh2 bilioni kwa ajili ya kumwezesha Zahera kutimiza majukumu yake kikamilifu.

“Natambua Zahera anahitaji zaidi ya Sh 1.5 bilioni kwa ajili ya kufanya usajili na hilo tunalifanyia kazi, lakini kwa hali ilivyo kwa sasa hata kama zitahitajika Sh2 bilioni, tutakuwa tayari. Soka linahitaji uwekezaji mkubwa na unapotaka kuwa na wachezaji wenye viwango vya kimataifa ni lazima gharama zihusika hapa.”