#KARIAKOODABI: Dante ana saa 72 kwa Kagere
Muktasari:
- Mlinzi wa Yanga, Andrew Vicent ‘Dante’ anafahamu kuwa mshambuliaji mahiri na nahodha wa Simba, John Bocco, hatakuwepo katika pambani la wa jadi litakalofanyika Septemba 30, lakini na anamjua vema Emmanuel Okwi, lakini bado hajaujua uchezaji wa Meddie Kagere, hivyo amejipa muda wa kumchunguza ili aweze kujua namna ya kumdhibiti watakapokutana Jumapili kwani mshambuliaji huyo pia ni hatari kwa kucheka na nyavu.
BEKI wa Yanga Andrew Vincent ‘Dante’ amesema taarifa za nahodha wa Simba, John Bocco kuukosa mchezo wa Septemba 30 ni habari njema kwao, lakini akafichua anamjua vyema Emmanuel Okwi na anataka kumsoma zaidi Meddie Kagere akitenga muda maalumu wa kufanya hivyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Dante alisema Bocco ni mshambuliaji aliyekamilika na kukosekana kwake katika mechi ya Jumapili wiki hii kutaipunguzia kazi safu yao ya ulinzi.
Dante alisema katika mastraika wa Simba waliosalia wote anawajua vyema na jinsi ya kuwazuia, lakini ni Kagere pekee anataka kumsoma zaidi akimtengea siku tatu sawa na masaa 72 za kumfuatilia.
Beki huyo alisema mbinu za kumzuia Okwi zipo ndani ya uwezo wao, ila atatumia muda wa siku tatu kujiongeza ili kujua mbinu za Kagere katika kufunga.
“Tumesikia kwamba Bocco amepata kadi nyekundu ni pigo kwao kutokana na Bocco sio mshambuliaji rahisi anajua kupambana na kufunga. Kagere analijua goli pia ana uzoefu aliposajiliwa Simba nilianza kumsoma taratibu, ila kwa siku hizi tatu hizi nataka kazi hiyo.”