Dante: Yanga ubingwa wetu Ligi Kuu
Muktasari:
- Harakati za kuwania ubingwa kwa msimu huu, zinaendelea huku timu tatu zikiwa zinapigiwa mahesabu ambazo ni Simba, Yanga na Azam FC ndicho alichozungumza beki wa Wanajangwani Andrew Vicent 'Dante'.
YANGA imefikisha pointi 71 kwa mechi 30 walizocheza, wameshinda 22, wana sare tano na wamefungwa michezo mitatu, kitu kilichomfanya beki wa timu Andrew Vicent 'Dante' kutamka kuwa anaamini wana nafasi kubwa ya ubingwa.
Mbio za ubingwa zinatazamwa kwenye klabu tatu, ambapo Yanga na Azam FC zote zimecheza mechi 30 isipokuwa zimetofautiana pointi, lakini Simba wao wamecheza michezo 22 ipo nafasi ya tatu kwa kumiliki pointi 57.
Dante ametazama utofautiano wa pointi na mechi, kisha akasema bado Yanga ina nafasi ya kuchukua ubingwa msimu huu, jambo kubwa analosema ni wao kushinda mechi nane zilizobakia.
"Hatutakiwi kuvipigia hesabu viporo vya Simba, tunapaswa kushinda mechi zilizobakia ili kuishi malengo yetu, Yanga tuna nafasi kubwa ya ubingwa kwani hakuna anayejua matokeo kabla ya mechi.
"Tumeshinda dhidi ya African Lyon ni kitu kizuri kwetu kwani kinakuwa kinaendelea kutuweka kwenye mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi kuu Bara.
"Lakini pia tunaelekeza nguvu kwenye michuano ya FA, kuhakikisha tunapata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mwakani,"anasema.