Bocco: Simba SC kuongoza ligi hatujabweteki mpaka kieleweke
Muktasari:
Simba kuongoza ligi haiwafanyi nyota wake waone wamemaliza kila kitu badala yake, John Bocco amesema wana kazi ngumu kufikia malengo yao.
Dar es Salaam. Pamoja na Simba SC kuongoza kwa pointi 53, haimfanyi nahodha wa timu hiyo John Bocco avimbe kichwa badala yake anaona wana kazi ngumu ya kulinda nafasi waliopo.
Bocco amesema kila timu inatamani kukaa kileleni na kwamba bado wana mechi 17 mkononi ambazo wanatakiwa kupambana kwa nguvu zote ili waweze kutetea ubingwa.
Amesema anaamini katika mshikamano kuanzia kwa wachezaji, mashabiki, viongozi na benchi la ufundi kwamba ndio silaha yakuwafanya watwae ubingwa.
"Ukisikia ubingwa maana yake kuna ushindani, anayefanya vyema ndiye anakuwa mbabe kuliko mwingine kwa sasa bado mechi zipo nyingi hivyo vita inaendelea,"
"Kila timu kwa sasa inaangalia Simba kuwa kileleni, hilo litafanya waibue ushindani mkali dhidi yetu, ndio maana nasema lazima tuongeze bidii ya kufikia malengo yetu,"amesema.
Mpaka sasa Bocco amefunga bao moja, kutokana na kukaa nje kwa muda mrefu akisumbuliwa na majeraha, amezungumzia hilo kwamba amerejea atapambana.
"Nilitamani kufanya makubwa, unajua Mungu ndiye anajua siri za maisha yetu, sikujua kama ningeumia, kubwa ninaloshukuru nimepona nitaendelea na majukumu yangu,"amesema Bocco.