Tshishimbi: Narudi kivigine mtaona ubora wangu
Muktasari:
Tshishimbi ni mchezaji pekee wa kigeni aliyeongezwa mkataba wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo kwa wachezaji waliomaliza mikataba ukiachana na Klaus Kindoki anayemaliza mkataba.
Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga Mkongomani Papy Tshishimbi amesema ametumia likizo yake kurudisha makali yake baada ya kumaliza msimu uliopita vibaya.
Tshishimbi anatarajia kutua nchini kesho tayari kwaajili ya kuingia kambini kujiandaa na mchezo wao wa kimataifa wa kirafiki maalum kwaajili ya kutambulisha wachezaji wapya unaotarajiwa kufanyika Agosti 3 Mwaka huu.
Tshishimbi alisema yupo fiti na amejiandaa kuhakikisha anacheza michezo yote ya ligi endapo atapewa nafasi na mwalimu huku akiomba Mungu kumuepusha na majeraha ya mara kwa mara kama ilivyokuwa msimu uliopita.
"Unajua ni ajabu sana mimi kucheza nusu dakika katika mchezo mimi nilivyokuwa nacheza Mbabane Swallows ya Swaziland, nakumbuka nilicheza dakika zote tisini michezo yote ya ligi na kucheza mashindano ya klabu bingwa hadi hatua ya makundi tuliyofika nilikosa mchezo mmoja tu nilikuwa na matatizo ya kifamilia."
"Huwezi kuamini siku nacheza na Simba mchezo wangu wa kwanza kabisa nimetua nilifanya mazoezi siku tatu tu na kiwango changu kilikuwa bora, lakini tangu hapo sielewi nilikumbwa na nini nikawa natolewa bila kumaliza dakika zote jambo ambalo lilikuwa kama suprise kwangu,"
"Sitaki hilo lijirudie tena nimetumia mapumziko vizuri kwa kufanya mazoezi mara mbili kwa siku asubuhi na jioni yote ni kuhakikisha najiweka fiti ili kulipa muda ambao sitajatumika mzunguko wa pili msimu ulioisha kuwaaminisha viongozi na mashabiki kuwa viongozi hawajakosea kuniongeza mkataba," alisema Tshishimbi.