Kagere jezi namba 14, mabao 14 anakitaka kiatu cha ufungaji bora Ligi Kuu
Muktasari:
Kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara hadi sasa ni Salim Aiyee wa Mwadui ambaye amepachika mabao 16
Morogoro. Mshambuliaji Meddie Kagere ametimiza mabao 14 yanayozidi kumweka kwenye nafasi nzuri ya kufukuzana na Salim Aiyee anayeongoza chati ya ufungaji wakati Simba ikichapa Mbao kwa magoli 3-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Kabla ya bao hilo ambalo Kagere alilifunga mnamo dakika ya 79 kwa mkwaju wa penalti, mshambuliaji huyo alikuwa amepachika mabao 13 ambayo yalikuwa ni matatu nyuma ya yale ya Aiyee wa Mwadui mwenye mabao 15 kwa sasa.
Penalti hiyo Kagere alipiga kwa ustadi mkubwa akimpoteza kipa kwa kukimbia na kusita kabla kupiga jambo lililomwacha kipa wa Mbao akiruka upande tofauti na mpira ulipoingia.
Penalti hiyo ilitokana na faulo ya beki Amimu Abdulkarim kumuangusha mshambuliaji Kagere ndani ya eneo la hatari la Mbao FC.
Bao hilo la Kagere lilikuwa ni kama sukari inayopakwa juu ya keki kwani tayari Simba ilikuwa imeshajihakikishia ushindi kupitia mabao mawili ya nahodha wao John Bocco.
Ni mchezo ambao sehemu kubwa ulitawaliwa na Simba ingawa kuna nyakati Mbao walijitahidi kulishambulia lango la wapinzani wao ingawa walikosa umakini wa kutumia nafasi walizopata.
Mwamuzi Erick Onoka kutoka Arusha aliwaonyesha kadi za njano wachezaji David Mwassa, Amimu Abdulkarim na Ally Musa wa Mbao kutokana na rafu walizocheza kwa wachezaji wa Simba.
Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe jumla ya pointi 57 zinazoifanya iendelee kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.