VIDEO: Yanga watishia kutinga mahakamani kuishtaki TFF, Karia

Muktasari:

Uchaguzi wa Yanga bado upo katika fukuto zito licha ya TFF kuendelea na mchakato lakini Yanga wamekuwa wakipinga uamuzi huo wakisema hawatashiriki hatua yoyote.

Dar es Salaam. Sekeseke la uchaguzi wa klabu ya Yanga limechukua sura mpya baada ya viongozi wa matawi kuanza kujipanga kwa lengo la kulishtaki mahakamani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Wakitangaza uamuzi huo leo Mwenyekiti wa Kamati ya Matawi Kanda ya Kinondoni, Shabani Huda amesema kwasasa wanajipanga kufungua kesi mahakamani kuwashtaki TFF kama ni haki yao kusimamia uchaguzi wa Yanga.

Mbali na Huda kiongozi mwingine wa tawi la Uhuru Kariakoo, Edwini Kaisi amesema katika uamuzi huo, watafungua kesi mbili ya kwanza kuomba tafsiri ya kisheria.

Kaisi amesema kesi ya pili itafunguliwa dhidi ya Rais wa TFF na katibu wake kwa uamuzi wao wa kumkataa Yusuf Manji kwa kuwa wao walishamhalalisha kuwa ni mwenyekiti wa Yanga.

Naye Mwenyekiti wa matawi kanda ya Temeke, Mustapha ameitaka Wizara ya Mambo ya Ndani chini ya Waziri Kangi Lugola na Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspector Simon Sirro kuwakamata wanachama wenzao Waziri Jitu na Ibrahim Akilimali kwa kitendo cha kuwatukana Rais John Pombe Magufuli na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika.

Mustapha amesema wiki iliyopita wawili hao walimkashifu Rais kwa wakidai hakufanya uamuzi sahihi kuchagua Mkuchika kuwa waziri kitendo ambacho ni kinyume na sheria ya nchi.