Mbelgiji Simba akabiziwa nyota wawili wa Gor Mahia

Muktasari:

Simba na Gor Mahia zote zinashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu

Dar es Salaam. Uongozi wa Simba umeanza kuichokoza Gor Mahia ya Kenya baada ya kukabidhi majina mawili ya Philemon Otien na Ephrem Guikan kwa kocha Mbelgiji Patrick Aussems.

Mbelgiji Aussems anataka kuimalisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji kutoka nje wakati wa dirisha dogo litakapofunguliwa Novemba 15.

Mbelgiji amekabidhiwa majina ya nyota hao wawili wa Gor Mahia, Mkenya Otien (26) anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji au mshambuliaji wakati Guikan anacheza katika nafasi ya ushambuliaji tangu alivyotua hapo msimu mmoja uliopita akitokea katika klabu ya AS Port Louis ya nchini Mauritius.

Guikan (24) raia wa Ivory Coast ailijiunga na Gor Mahia mwanzo wa msimu uliopita kwa maana hiyo mkataba wake umebaki mwaka mmoja na ameweza kuifungia timu yake mabao 17 msimu mzima katika mashindano yote.

Simba wanaingia katika vita ya kumuania Guikan dhidi ya timu mbili kubwa Afrika ambazo ni Free State Stars ya Afrika Kusini na Nkana Fc inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Zambia.

Wakala wa Guikan, George Bwana aliweka wazi kuwa amezungumza na uongozi wa Simba na kweli wameonesha nia ya kumtaka nyota wake huyo ambaye amebakisha mwaka mmoja wa kuitumia klabu ya Gor Mahia ambayo kesho Jumanne inacheza na Everton nchini Uingereza.

Bwana alisema aliwasiliana na kiongozi wa juu wa Simba ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi kuwa wanamuhitaji Guikan, lakini bado hawajafikia uamuzi ya mwisho ya kumchukua kwani bado wapo katika majadiliano.

"Kiongozi huyo wa Simba aliniambia wanamtaka mchezaji wangu Guikan, lakini anasubiri wa kufanya uamuzi wamalizana naye," alisema.

"Kwangu sina shida nawasubiri Simba maana ni timu nzuri, lakini hapa mkononi nipo na ofa kutoka Nkana na Free State zinamtaka mchezaji wangu nimewambia wasubili kwanza nioni hili la Simba tutalimaliza vipi," alisema Bwana.

Kocha wa Simba, Aussems awali aliweka wazi kwamba yupo na orodha ya wachezaji watano mpaka sita ambayo atawapatia kamati ya usajili ili waweze kumsajili nyota mmoja na kama wao watapenda kumuongeza mwingine mwenye uwezo halitakuwa na shida kwake.

"Nataka straika mwenye uwezo wa kufunga kama waliokuwa sasa au zaidi yao lakini awe na uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga kwa wenzake," alisema Aussems.

Sifa hizo ambazo Aussems ameziweka hapo kwa straika ambaye anamuhitaji zinapatikana kwa Guikan na huenda Simba wakaingia miguu miwili kumalizana na straika huyo.