Yanga, GSM wahujumiwa jezi

KAMPUNI ya GSM inayodhamini klabu ya Yanga imedai kuhujumiwa baada ya kuwepo wajanja wanaouza jezi bandia za timu hiyo.

Kutokana na kuwepo kwa wafanyabiashara hao jijini Mbeya, uongozi wa GSM Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa kushirikiana na Polisi juzi walifanya msako kwenye maduka na kukamata jezi feki zikiwa sokoni.

Meneja Mauzo wa GSM wa kanda hiyo, Jumanne Nango alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wapenzi wa Yanga kwamba kuna jezi feki zinauzwa mtaani ndipo wakaingia mtaani na kufanya msako.

“Mashabiki wa Yanga wakauliza kwa nini nyie (GSM) dukani kwenu mnauza jezi bei ghali zaidi wakati tukienda mtaani huko tunauziwa bei ya Sh10,000 hadi 15,000 jezi za Yanga,” alisema Nango.

“Jezi halisi dukani inauzwa Sh40,000 lakini wajanja huko mitaani wanauza kati ya Sh10,000 na 15,000, sasa unaweza kuona hujumu hapa ni kubwa sana kwa klabu.

“Kwa kushirikiana na Polisi tumekamata jezi feki 59 kwenye maduka tofauti na watuhumiwa wawili wanashikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi.”

Nango alisema kuwa wajanja hao wametengeneza jezi za aina tofauti zikiwemo za watoto ambazo hata GSM hawajatengeneza wala kuingiza sokoni.

Mfanyabiashara wa vifaa vya michezo Kabwe jijini Mbeya, Alfredy Nsega maarufu kama Uefa Shop, alisema kuwepo kwa jezi feki kunawarudisha nyuma kimaslahi.