Wirtz kashuka zaidi, Cherki amepaa EPL
Muktasari:
- EPL yenye timu 20 asilimia 72.1 ya wachezaji katika ligi hiyo (takriban 391) ni wa kigeni ilhali 27.9 ni wazawa, huku wastani wa umri wa nyota wote wanaocheza michuano hiyo ukiwa ni miaka 26.2. Hata hivyo, katika tathmini iliyofanywa na Tranfermark majuzi inaonyesha kwamba mastaa 257 wamepandisha thamani ya ligi kwa Euro 945 milioni na kufikia Euro 4.10 bilioni.
LONDON, ENGLAND: MASTAA 257 kati ya 542 wanaokipiga katika katika Ligi Kuu England (EPL), wamefanyiwa tathmini ya kuangalia thamani zao upya baada ya kucheza raudi sita za msimu wa 2026/27.
EPL yenye timu 20 asilimia 72.1 ya wachezaji katika ligi hiyo (takriban 391) ni wa kigeni ilhali 27.9 ni wazawa, huku wastani wa umri wa nyota wote wanaocheza michuano hiyo ukiwa ni miaka 26.2. Hata hivyo, katika tathmini iliyofanywa na Tranfermark majuzi inaonyesha kwamba mastaa 257 wamepandisha thamani ya ligi kwa Euro 945 milioni na kufikia Euro 4.10 bilioni.
Katika tathmini mpya ya Transfermarkt ya thamani za wachezaji hao kwa Oktoba 2026 inaonyesha kwamba kiungo wa Liverpool, Florian Wirtz, ameshuka thamani zaidi na Rayan Cherki wa Manchester City akiwa miongoni mwa vinara wa ongezeko hilo.
Enzo, Anderson na Rogers si mchezo
Dirisha la usajili la majira ya kiangazi lilishuhudia klabu za Ligi Kuu England zikitumia kiasi kikubwa cha fedha, huku baadhi zikilipa ada kubwa kusajili nyota mbalimbali. Ben Littlemore, mratibu wa tathmini za thamani za Ligi Kuu England wa Transfermarkt, anasema kulikuwa na ongezeko la ada za uhamisho, hasa kwa wachezaji waliokuwa tayari na uzoefu wa kucheza katika ligi hiyo. Hali hiyo imechangia kupanda kwa thamani za wachezaji kadhaa katika tathmini ya Oktoba.
Kiungo Enzo Fernandez wa Manchester City amepanda kwa Euro 20 milioni na kufikia Euro 120 milioni. Nyota mwenzake wa City, Elliot Anderson na Morgan Rogers wa Chelsea nao wamefikia kiwango hicho baada ya thamani zao kuongezeka kwa Euro 10 milioni kila mmoja.
Watatu hao sasa wanaungana na Declan Rice wa Arsenal ambaye thamani yake ni Euro 120 milioni, wakiwa miongoni mwa wachezaji wenye thamani kubwa zaidi katika ligi hiyo nyuma ya Erling Haaland wa Manchester City.
Littlemore anakiri kuwa ada zilizolipwa kwa Fernandez, Anderson, Rogers na wachezaji wengine katika dirisha la usajili zilionekana kuwa kubwa kupita kiasi. Hata hivyo, tathmini inapaswa kuzingatia mabadiliko ya soko pamoja na mwanzo mzuri wa wachezaji hao katika timu zao mpya.
Cherki na Pedro waongoza ongezeko
Wachezaji 10 wamepata ongezeko la thamani la Euro 20 milioni kila mmoja katika tathmini hiyo. Mbali na Fernandez na Cherki, wengine ni Joao Pedro wa Chelsea, Mateus Fernandes wa Tottenham Hotspur, Alex Scott wa Bournemouth, Myles Lewis-Skelly wa Arsenal, Matias Fernandez-Pardo wa Newcastle United, Max Dowman wa Arsenal, Rio Ngumoha wa Liverpool na Ibrahim Mbaye wa Aston Villa.
Baada ya ongezeko hilo, Cherki sasa ana thamani ya Euro 110 milioni, huku Pedro akifikia Euro 100 milioni. Mateus Fernandes na Alex Scott wana thamani ya Euro 70 milioni kila mmoja, wakati Lewis-Skelly amefikia Euro 65 milioni. Harrison Armstrong wa Everton ana ongezeko la Euro 18 milioni na kufikia Euro 30 milioni, huku straika mpya wa Ipswich Town, Emersonn akipanda kwa Euro 17 milioni na kufikia Euro 25 milioni.
Littlemore anasema Cherki ameendelea kuonyesha kiwango bora katika Ligi Kuu England na kuongeza mchango wake wa takwimu, akisisitiza kuwa sasa anahesabiwa miongoni mwa wachezaji bora wa ligi hiyo.
Kuhusu Pedro, anasema mshambuliaji huyo alianza msimu kwa kiwango kizuri licha ya kutokuwamo katika kikosi cha Brazil cha Kombe la Dunia. Kwa mujibu wa takwimu, Pedro alikuwa amehusika moja kwa moja katika mabao sita katika mechi nne za Chelsea.
Littlemore pia anamsifu Scott kwa kuanza msimu vizuri na kupata nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza katika timu ya taifa ya England. Kwa upande wa Lewis-Skelly, kiungo huyo ameonyesha kuwa anaweza kucheza vizuri katikati ya uwanja na kupata nafasi katika kikosi cha Arsenal.
Wirtz ashuka kwa Euro 15 milioni
Wakati baadhi ya mastaa wakipanda thamani, Florian Wirtz wa Liverpool ndiye aliyeshuka zaidi, ambapo kiungo huyo Mjerumani ametoka Euro 100 milioni hadi milioni 85. Tangu alipohamia England, thamani yake imeshuka kutoka Euro milioni 140 hadi milioni 85.
Littlemore anasema awali Transfermarkt ilizingatia uwezekano wa Wirtz kuhitaji muda kuzoea Ligi Kuu England kutokana na aina yake ya uchezaji. Hata hivyo, kiwango anachoonyesha bado hakijafikia matarajio ya mchezaji mwenye thamani kubwa kiasi hicho.
Wachezaji wengine walioshuka thamani kwa Euro milioni 10 kila mmoja ni Martín Zubimendi na Viktor Gyokeres wa Arsenal, pamoja na Richarlison wa Tottenham Hotspur.
Na katika hilo, Littlemore anasema Gyokeres amepunguziwa thamani kwa kiasi kikubwa kwa sababu sasa anaonekana kuwa chaguo la pili katika nafasi ya mshambuliaji wa Arsenal pale Kai Havertz anapokuwa fiti na pia anapoingia akitokea benchi hana kiwango cha kutisha.
Kwa upande wa Zubimendi, anasema tathmini ilikuwa ngumu zaidi kwa sababu kiwango chake kimeendelea kuwa kizuri na bado kuna mahitaji ya soko kwake. Hata hivyo, ushindani mkubwa wa nafasi katika kikosi cha Arsenal umepunguza nafasi yake katika mpango wa timu.
Ngumoha, Dowman uwezo wa kizazi kipya
Wachezaji wenye umri mdogo Rio Ngumoha (18) wa Liverpool na Max Dowman (16) wa Arsenal ni miongoni mwa wanaovutia zaidi katika tathmini hiyo, ambapo thamani ya kila mmoja imeongezeka kutoka Euro 30 milioni hadi Euro 50 milioni, ikiwa ni ongezeko la Euro 20 milioni.
Littlemore anasema Transfermarkt imekuwa ikiona mwelekeo wa klabu kuwa tayari kutumia fedha nyingi kuwasajili wachezaji wadogo zaidi, hivyo imeamua kufanya tathmini ya thamani zao kwa kuzingatia uwezo wao wa baadaye.
Anasema Ngumoha tayari anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara Liverpool na hivi karibuni alipata katika timu ya taifa ya England. Kwa upande wa Dowman, klabu inadhibiti muda wake wa kucheza kutokana na umri wake, lakini kila anapopata nafasi amekuwa akivutia na anaonekana kuwa mchezaji mwenye kipaji cha kipekee kwa kizazi chake.