Vita ndogo Ulaya, Brighton ikipigiwa upatu kutwaa taji Conference League
Muktasari:
- Hatua ya ligi katika mashindano hayo ina michezo sita kwa kila timu badala ya minane, hivyo, wakati Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Europa tayari zikiingia raundi ya pili ya michezo, Conference ndiyo inaanza leo, Alhamisi, Oktoba 15, 2026.
LONDON, ENGLAND: KAMA ilivyokuwa Ligi ya Mabingwa Ulaya jana na juzi, Ligi ya Europa, Conference zinaendelea leo huku kila moja ikiwa na timu 36 zinazoshiriki.
Hatua ya ligi katika mashindano hayo ina michezo sita kwa kila timu badala ya minane, hivyo, wakati Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Europa tayari zikiingia raundi ya pili ya michezo, Conference ndiyo inaanza leo, Alhamisi, Oktoba 15, 2026.
Mataji mawili kati ya matatu yaliyopita ya Conference League yamechukuliwa na timu za England, huku Crystal Palace ikitwaa lake la kwanza la Ulaya Mei, mwaka huu baada ya kuifunga Rayo Vallecano katika fainali.
Je, wapinzani wao wakubwa Brighton wataifanya Ligi Kuu England kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo, au timu nyingine itajitokeza na kufanya vizuri? Opta imefanya tathmini na kuibuka na utabiri wa timu zenye uwezekano mkubwa wa kufanya vizuri na kutinga fainali itakayochezwa Istanbul, Uturuki, Juni 2, 2027.
NAFASI KUBWA KUBEBA CONFERENCE LEAGUE
Licha ya kutowahi kutwaa taji lolote la mashindano ya Ulaya, Brighton inapewa nafasi kubwa ya kutwaa Conference League msimu huu kabla hata ya mpira kuanza kuchezwa. Kuna sababu nyingi zinazoifanya Opta kuipa Brighton nafasi hiyo, lakini kubwa ni nafasi yake ya juu katika viwango vya sasa vya ushindani ikilinganishwa na timu nyingine shiriki katika mashindano hayo.
Kutokana na kufanya vizuri katika ligi yenye ushindani mkubwa zaidi duniani, kwa mujibu wa viwango vya Opta, pamoja na kuanza vizuri msimu huu katika Ligi Kuu England ikiwamo ushindi mkubwa wa mabao 3-0 dhidi ya Arsenal inayoshika nafasi ya kwanza katika viwango hivyo duniani, Brighton inashika nafasi ya saba katika viwango vya kimataifa vya Opta.
Nafasi hiyo inaiweka mbele ya timu kama Real Madrid, Inter Milan na Manchester United, ikiwa ya pili tu nyuma ya PSG, mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler atalazimika kuiongoza timu hiyo katika mashindano ya Ulaya sambamba na Ligi Kuu England, huku uwezo wa kumudu michezo ya ziada utakuwa muhimu kuifanya isiyumbe katika mashindano yote mawili.
Kwa mujibu wa Opta, Brighton ina nafasi kubwa ya kwenda mbali katika mashindano ya Ulaya ikipewa asilimia 44.5 kutwaa Conference League msimu huu. Klabu hiyo ya pwani ya kusini mwa England ina uwezekano wa asilimia 98.2 wa kufuzu hatua ya 16 bora.
Hata hivyo, kuna timu nyingine zinazoweza kufanya vizuri endapo Brighton itakwama; Monaco ikiwa pia imeanza vizuri msimu wa Ligi Kuu Ufaransa ikiwa kileleni mwa Ligue 1 baada ya kucheza michezo sita, huku ikitumia vibaya hali ya kutokuwa na matokeo mazuri kwa PSG.
Kocha wa kikosi hicho, Filipe Luis amekifanya kucheza soka zuri, na uzoefu wao mkubwa zaidi katika mashindano ya Ulaya unaweza kuwapa faida dhidi ya Brighton, ambayo watakutana nayo nyumbani katika siku ya tano ya michezo ya hatua ya ligi. Opta inaipa Monaco uwezekano wa asilimia 9.7 wa kutwaa Conference league, ikiwa mbele kidogo ya Freiburg, ambayo pia imepangiwa kukutana nayo.
Timu hiyo ya Bundesliga ilifungwa na Aston Villa katika fainali ya Ligi ya Europa msimu uliopita, lakini itatumia mashindano hayo kujaribu kurekebisha makosa ikiwa miongoni mwa zinazopigiwa upatu zaidi, ikishika nafasi ya tatu. Kama ilivyo Monaco, Freiburg inaongoza Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) kwa namna ambayo haikutarajiwa na wengi. Freiburg, inayojulikana pia kwa jina la Breisgau Brazilians, inapewa asilimia 9.3 kutwaa Conference League.
NYINGINE HIZI HAPA
Timu nyingine iliyopata mafanikio makubwa katika misimu ya hivi karibuni ya Ligi ya Europa ni Atalanta maarufu kama La Dea iliyotwaa taji msimu wa 2023/24. La Dea ilishiriki Ligi ya Mabingwa msimu uliopita na kufika hatua ya 16 bora, lakini ilitupwa nje na Bayern Munich kwa jumla ya mabao 10-2.
Hata hivyo, haitalazimika kukutana na timu yenye kiwango cha Bayern katika mashindano Conference League, na ina uwezekano wa asilimia 6.9 wa kuongeza taji la ligi hiyo katika mafanikio yake ya awali ya kutwaa Ligi ya Europa. SC Braga inafuata, ingawa imeanza kwa matokeo yasiyoridhisha katika Ligi Kuu Ureno Primeira Liga, ikiwa imeshinda michezo mitatu kati ya saba ya mwanzo, sare mbili na kupoteza miwili.
Braga ilifungwa na Freiburg katika nusu fainali ya Ligi ya Europa msimu uliopita, lakini inapewa asilimia 4.2 wa kutwaa Conference League.
Timu nyingine mbili pekee zenye uwezekano wa angalau asilimia tatu wa kutwaa taji hilo ni Midtjylland yenye asilimia 3.5 na FC Copenhagen yenye asilimia tatu zote za Denmark. Asilimia nyingine zinazostahili kuangaliwa ni za Ajax, iliyotwaa Kombe la Ulaya/Ligi ya Mabingwa mara nne, yenye uwezekano wa asilimia 2.1 na Trabzonspor anayoichezea nyota wa Misri, Mohamed Salah yenye asilimia 1.1.
Majina hayo makubwa katika soka, Ajax na Salah, huenda hayapo katika kiwango cha juu kama ilivyokuwa zamani, lakini yana uwezo wa kufanya mambo ya kushangaza. Hearts ambayo ilikaribia sana kuvunja utawala wa Glasgow katika Ligi Kuu Scotland msimu uliopita, lakini sasa imepata nafasi ya kujitambulisha zaidi katika mashindano ya Ulaya. Klabu hiyo ya Edinburgh inapewa asilimia 0.1 kutwaa Conference League. Hata hivyo, ina uwezekano wa asilimia 20.7 wa kufika hatua ya 16 bora.
Kuna timu tano ambazo hazipewi nafasi kutwaa Conference League ambazo ni KF Egnatia, Iberia 1999, Inter Club d’Escaldes, Kauno Zalgiris na Lincoln Red Imps. Pamoja na mechi za Conference League, zile za Europa pia zinapigwa leo katika viwanja mbalimbali Ulaya.
CONFERENCE LEAGUE LEO, ALHAMISI
Universitatea Craiova v Getafe
Gent v AGF
Hajduk Split v Ajax
KF Egnatia v FC Midtjylland
KuPS v Trabzonspor
Lugano v FK Crvena Zvezda
Mjaellby v Inter Club d’Escaldes
Panathinaikos v Borac Banja Luka
PFC CSKA Sofia v AS Monaco
Riga FC v Kairat Almaty
Atalanta v Pafos FC
Brann v Lincoln Red Imps FC
Brighton v FK Kauno Zalgiris
FC Copenhagen v SC Braga
FC Twente v Thun
Freiburg v Jablonec
Hearts v FC Nordsjaelland
St.Truiden v FC Iberia 1999