Vigogo Man United waulizia kuhusu Christopher Nkunku
Muktasari:
- Garnacho hivi karibuni amekuwa hapati nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha Man United baada ya kocha wa timu hiyo kuweka wazi kwamba haridhishwi na utendaji kazi wake.
MANCHESTER United imeulizia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Chelsea na Ufaransa, Christopher Nkunku, 27, kwa ajili ya kuziba pengo la winga wao raia wa Argentina, Alejandro Garnacho, 20, ambaye anahusishwa sana na Chelsea tangu kuanza kwa wiki iliyopita.
Garnacho hivi karibuni amekuwa hapati nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha Man United baada ya kocha wa timu hiyo kuweka wazi kwamba haridhishwi na utendaji kazi wake.
Licha ya kutopata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Chelsea hususani katika mechi za ligi, Nkunku ni miongoni mwa washambuliaji wa timu hiyo wanaoongoza kwa mabao akitupia kambani mara nane na kutoa asisti tano.
Katika mabao hayo manane ni matatu tu ndio amefunga kwenye EPL na yaliyobakia alifunga katika michuano ya kimataifa, Carabao na FA. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Marcus Rashford, 27, amepanga kukubali kupunguziwa mshahara ili kukamilisha dili lake la kujiunga na Barcelona katika dirisha hili la majira ya baridi.
Awali, ilielezwa kwamba mabosi wa Barcelona wanataka kuachana na mchakato wa kumsajili fundi huyu kwa sababu kanuni za La Liga haziwaruhusu kumsajili na kumpa mshahara anaopata kwa sasa au hata nusu yake.
MKURUGENZI wa Napoli, Giovanni Manna amethibitisha kuwa ni kweli wanahitaji huduma ya mshambuliaji wa Borussia Dortmund na Ujerumani, Karim Adeyemi, 23, katika dirisha hili lakini haitolipa kiasi kikubwa cha pesa kukamilisha usajili wake.
Adeyemi ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu huu amecheza mechi 14 za michuano yote na kufunga mabao matano.
MANCHESTER United imewasilisha ofa mpya ya Pauni 27 milioni kwenda Lecce ili kuipata huduma ya beki wa kushoto wa timu hiyo, Patrick Dorgu, 20, baada ya ofa yao ya kwanza kukataliwa.
Hata hivyo, ofa hiyo mpya pia imekataliwa na Lecce imesisitiza kwamba inahitaji Pauni 35 milioni ili kumuuza. Mkataba wake unamalizika mwaka 2029.
NEWCASTLE United inajiandaa kumpa ofa ya mkataba moya straika wao raia wa Sweden, Alexander Isak utakaomfanya asalie kwenye viunga hivyo kwa muda mrefu zaidi.
Isak ni mmoja kati ya mastaa wanaowindwa na timu nyingi barani Ulaya kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Mkataba wa Isak unatarajiwa kuamlizika mwaka 2028.
REAL Madrid imeingia kwenye vita dhidi ya Paris St-Germain na Al-Nassr ili kuipata saini ya straika wa Aston Villa na Colombia, Jhon Duran, 21, katika dirisha hili.
Duran amekuwa katika rada za timu nyingi barani Ulaya kutokana na kiwango bora alichoonyesha hususani msimu huu akiwa na Villa ambapo amefunga mabao 12 katika mechi 28 za michuano yote.
STRAIKA wa RB Leipzig na Slovenia, Benjamin Sesko, 21, anatamani zaidi kutua Arsenal badala ya Chelsea au Manchester United ambazo zote zinataka kumsajili katika dirisha hili.
Licha ya timu nyingi kutamani kumsajili Januari hii, mabosi wa Leipzig wamesisitiza kwamba hawana mpango wa kumuuza kwa sasa na badala yake watasubiri hadi mwisho wa msimu.
KOCHA wa Fenerbahce, Jose Mourinho wamewasilisha jina la winga wa Barcelona na Hispania, Ansu Fati, 22, anayetaka asajiliwe katika dirisha hili kwa mkopo ili kuongeza nguvu kwenye eneo lake la ushambuliaji.
Fati anatajwa kuwa katika orodha ya kuondoka Barca katika dirisha hili kwa sababu hayupo katika mipango ya kocha Hans Flick.