Vigogo Madrid watua kwa Diogo Dalot
Muktasari:
- Mkataba wa staa huyu wa kimataifa wa Ureno unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na msimu huu amecheza mechi 21 za michuano yote na kutoa asisti mbili.
REAL Madrid imefanya mawasiliano na wawakilishi wa beki wa pembeni wa Manchester United, Diogo Dalot, 25, kwa ajili ya kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi na imeandaa ofa ya Pauni 41.5 milioni.
Mkataba wa staa huyu wa kimataifa wa Ureno unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na msimu huu amecheza mechi 21 za michuano yote na kutoa asisti mbili.
Licha ya kutaka kumsajili Dalot, Madrid pia bado ina mpango wa kutaka kuipata huduma ya beki wa Liverpool, Trent Alexander Arnold ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Katika siku chache zilizopita Madrid iliripotiwa kuwasiliana na Liverpool kuwapa taarifa kwamba wanataka kuzungumza na Trent ambaye inaweza kumsainisha mkataba wa awali Januari mwakani.
Kwa upande wa Dalot, inaonekana itakuwa ngumu kumpata kutokana na umuhimu wake katika kikosi cha kwanza cha Man United.
Mohamed Salah
RIPOTI za ndani kutoka Liverpool zinadai winga wa timu hiyo na Misri, Mohamed Salah yupo tayari kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kusalia kwenye viunga hivyo, lakini hadi sasa bado hajapokea ofa yoyote kutoka kwa vigogo wa timu hiyo. Salah ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu amekuwa akihusishwa na timu kubwa za Saudi Arabia.
Amad Diallo
KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amependekeza winga wa timu hiyo na Ivory Coast, Amad Diallo asainishwe mkataba mpya wakati ule wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu. Diallo mwenye umri wa miaka 22, ni mmoja wa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Man United na msimu huu ameonyesha kiwango bora.
Leroy Sane
BAYERN Munich imeanza mazungumzo na wawakilishi wa winga wao raia wa Ujerumani, Leroy Sane, 28, ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Tangu dirisha lililopita Sane amekuwa akihusishwa kuondoka Bayern na timu mbalimbali zimekuwa zikihusishwa kutaka kumsajili na miongoni mwa hizi ni Barcelona.
Raul Asencio
REAL Madrid imepanga kumpa ofa ya mkataba mpya beki wao kijana raia wa Hispania, Raul Asencio, 21, katika siku chache zijazo. Asencio ni miongoni mwa wachezaji vijana walioonyesha kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu na amecheza mechi 15 za michuano yote. Mkataba wa sasa wa Raul unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Arda Guler
Arsenal bado imeendelea kuwa na matumaini ya kumsajili kiungo wa Real Madrid na Uturuki, Arda Guler, 19, dirisha lijalo. Guler anatajwa kutaka kuondoka Madrid tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Madrid. Licha ya kuonyesha nia ya kutaka kumsajili, ripoti zinaeleza benchi la ufundi la Madrid halihitaji kuona staa huyo anauzwa.
Dusan Vlahovic
Arsenal bado ina mpango wa kumsajili straika wa Juventus na Serbia, Dusan Vlahovic, 24, dirisha lijalo la majira ya baridi au kiangazi ili kuboresha eneo lao la ushambuliaji.
Dusan ni mmoja kati ya mastaa tegemeo kikosi cha kwanza cha Juventus na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 16 za michuano yote na kufunga mabao tisa, pia ametoa asisti moja.
Dominic Calvert-Lewin
BESIKTAS imeanza mazungumzo na wawakilishi wa straika wa Everton, Dominic Calvert-Lewin ili kuipata saini yake dirisha la majira ya baridi mwakani na atakuwa amebakisha miezi sita. Mbali ya Besiktas huduma ya Lewin mwenye umri wa miaka 27, pia inawindwa na Newcastle, Arsenal na Manchester United zinazopanga kumsajili mazima. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.