Vigogo Arsenal wajitosa dili la Dani Olmo
Muktasari:
- Olmo atakuwa mchezaji huru ifikapo Januari 1, ikiwa Barcelona haitafanikiwa kurefusha muda wake katika mfumo.
ARSENAL imeingia katika vita ya kutaka kumsajili kiungo wa Barcelona, Dani Olmo katika dirisha lijalo la majira ya baridi ambapo itatakiwa kuzipiku Manchester City na Manchester United zilizodaiwa kukutana na wakala wake siku kadhaa zilizopita.
Olmo atakuwa mchezaji huru ifikapo Januari 1, ikiwa Barcelona haitafanikiwa kurefusha muda wake katika mfumo.
Awali staa huyu alipewa usajili wa muda ili aitumikie Barca hadi mwisho wa mwaka kutokana na hali mbaya ya kiuchumi inayopitia.
Baada ya usajili huo wa muda, mamlaka za soka nchini Hispania zinaitaka Barca kuwasilisha vielelezo vinavyoonyesha kwamba uchumi wake umeinuka ili ipewe ruhusa ya kumuingiza katika mfumo rasmi na kumtumia hadi mwisho wa msimu.
Barcelona imewasilisha maombi mara mbili kuonyesha uchumi umeimarika na wanahitaji kurefusha muda wa Olmo kuwatumikia, lakini La Liga imetupilia mbali maombi hayo kwa sababu imeona uchumi wa timu hiyo haujaimarika.taba wa sasa wa Olmo unatarajiwa kumalizika mwaka 2030, lakini kama itashindikana Barca kurefusha muda wake katika mfumo, atakuwa huru kuondoka akiwa mchezaji huru ifikapo Januari Mosi.
MANCHESTER City inapambania uwezekano wa kumsajili kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi katika dirisha lijalo ambapo ipo tayari kutoa Pauni 50 milioni kwa ajili ya kukamilisha mchakato huo. Man City inataka kumsajili Zubimendi ili kuziba pengo la kiungo Mhispania Rodri ambaye atakuwa nje kwa msimu mzima. Mkataba wa sasa wa Zubimendi unatarajiwa kumalizika 2027.
JUVENTUS imekataa kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na England, Marcus Rashford, 27, licha ya kupewa ofa ya kufanya hivyo na wawakilishi wake na badala yake inaitaka huduma ya mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Joshua Zirkzee, 23. Inaelezwa Zirkzee ni pendekezo la kocha Thiago Motta ambaye alikuwa akitamani huduma tangu mchezaji huyo alipokuwa akiitumikia Bologna katika Ligi Kuu Italia (Serie A).
LIVERPOOL, Real Madrid, Manchester City na Paris St-Germain zote zipo katika vita kali ya kutaka kumsajili kiungo wa Bayern Munich na Ujerumani, Jamal Musiala, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Musiala ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao, msimu huu amecheza mechi 22 za michuano yote na kufunga mabao 14.
KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim anadaiwa kuitamani huduma ya straika wa PSG, Mfaransa Kolo Muani, 26, katika dirisha lijalo la majira ya baridi licha ya ushindani mkali uliopo kutoka Chelsea, Tottenham Hotspur na Arsenal. Muani ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika amepewa ruhusa ya kuondoka dirisha lijalo akipata timu itakayoumnunua.
LIVERPOOL bado inahitaji kumsajili mshambuliaji wa Inter Milan na Ufaransa, Marcus Thuram, 27, ambaye katika mkataba wake ana kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu inayomtaka italipa Pauni 70.5 milioni. Marcus ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha Inter Milan na msimu huu amecheza mechi 21 za michuano yote na kufunga mabao 13.
ARSENAL huenda ikamsajili straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres dirisha la majira ya baridi badala ya kiangazi baada ya kuumia Bukayo Saka aliyepata majeraha yatakayomuweka nje ya uwanja zaidi ya miezi miwili. Gyokeres anayehusishwa na timu nyingi Ulaya tangu dirisha lililopita, alidaiwa kuwa anaweza kuondoka lakini hadi mwisho wa msimu.
MABOSI wa Wolves wamesisitiza hawana mpango wa kumuuza mshambuliaji Mbrazili Matheus Cunha, 25, katika dirisha lijalo licha ya timu mbalimbali ikiwamo Arsenal na Manchester United kuonyesha nia ya kutaka kumsajili.Cunha mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027. Msimu huu amecheza mechi 19 na kufunga mabao 10.