Tottenham, Arsenal zapania kuinasa saini ya Nico Williams
Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya Fichajes, kiasi hicho cha pesa kimewekwa katika mkataba wake kama bei kwa timu yoyote inayohitaji huduma yake.
TOTTENHAM na Arsenal zipo tayari kulipa Euro 58 milioni Athletic Bilbao kwa ajili ya kuipata saini ya winga wa timu hiyo na Hispania, Nico Williams.
Kwa mujibu wa tovuti ya Fichajes, kiasi hicho cha pesa kimewekwa katika mkataba wake kama bei kwa timu yoyote inayohitaji huduma yake.
Katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, fundi huyu alikuwa akihusishwa sana na Barcelona.
Timu nyingi zilivutiwa naye kutokana na kiwango bora alichoonyesha kwenye michuano ya Euro iliyopita akiwa na Hispania iliyochukua ubingwa.
Msimu huu pia ameanza na moto La Liga na michuano mbalimbali aliyocheza na hadi sasa amecheza mechi 29 za michuano yote na kufunga mabao matatu.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na Bilbao pia inapambana ili kumsainisha mkataba mpya.
BAYER Leverkusen imefanya mawasiliano na Manchester City ili kuulizia uwezekano wa kuipata saini ya straika wa timu hiyo raia wa England, James McAtee, 22, kwa mkopo. James ambaye sio chaguo la kwanza la Pep Guardiola ameruhusiwa kuondoka na benchi la ufundi la timu hiyo ikiwa atahitaji kufanya hivyo. Mkataba wake wa mkopo unaweza kuwa na kipengele cha kumnunua mazima kwani kuna uwezekano mdogo akarudi City.
IMEFICHUKA Al Nassr ya Saudi Arabia ipo tayari kutoa Euro 100 milioni kwenda Aston Villa ili kuipata saini ya straika wa timu hiyo na timu ya taifa ya Colombia, Jhon Duran, 21, dirisha hili. Al Nassr inapambana kusajili mshambuliaji ambaye ataenda kucheza na Ronaldo katika safu ya ushambuliaji. Duran amevutia Waarabu hawa baada ya kiwango bora alichoonyesha hususani msimu huu na wanaamini kiasi hicho cha pesa kitamvutia kwenda kucheza Saudi Pro League.
MANCHESTER United imepanga kumsajili mshambuliaji wa Chelsea na Ufaransa, Christopher Nkunku, 27, kama Marcus Rashford ataondoka dirisha hili. Rashford anahusishwa sana na Barcelona ambayo bado ina suasua kumsajili kwa sababu inahitaji kuondoa wachezaji kabla ya kumchukua. Dili la Nkuku ambaye hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Chelsea linatarajiwa kuwa kwa mkopo wa nusu msimu.
CHELSEA imewekeza nguvu zaidi katika harakati za kutaka kumsajili mshambuliaji wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, 21, pamoja na staa wa Bayern Munich Mathys Tel, 19, katika dirisha hili baada ya kukubaliana lengo mama kwa sasa ni kuboresha zaidi safu yao ya ushambuliaji badala ya ulinzi kama ilivyokuwa hapo awali. Katika dili la Sesko, kumekuwa na ugumu kutokana na uwepo wa timu nyingine zinazomhitaji ikiwemo Man United.
KIUNGO wa Chelsea na Italia, Casare Casadei, 22, yupo kwenye hatua za mwisho kujiunga na Lazio ya Italia kwa ada ya uhamisho ya Pauni 11 milioni katika dirisha hili. Casadei aliomba mwenyewe kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Chelsea, hivyo anahitaji changamoto mpya sehemu nyingine. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
BRENTFORD imempa ofa beki wa Barcelona, Andreas Christensen, 28, kujiunga nao dirisha hili la majira ya baridi ambapo amehakikishiwa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza. Hata hivyo, fundi huyu wa Denmark amekataa na kusisitiza bado anatamani kuendelea kuitumikia Barca na kupambania namba kikosi cha kwanza.
WOLVES na Leicester City zinafikiria kumsajili kiungo wa Besiktas na England, Alex Oxlade-Chamberlain, 31, katika dirisha hili. Staa huyu ambaye hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Besiktas yupo tayari kuondoka kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine na timu hizo za England zinawania kuipata saini yake.