Staa anayesakwa Man United atakavyoleta utamu kikosini
Muktasari:
- Amorim ameshikilia msimamo wake wa kutumia fomesheni anayoipenda ya 3-4-3 tangu alipotua Old Trafford, Novemba mwaka jana.
MANCHESTER, ENGLAND: ACHA shoo ianze tuone. Hicho ndicho unachoweza kusema baada ya kuelezwa kwamba, mchezaji Patrick Dorgu anaweza kuwa majibu ya shida nyingi zinazomkabili kocha Ruben Amorim kwenye kikosi cha Manchester United.
Amorim ameshikilia msimamo wake wa kutumia fomesheni anayoipenda ya 3-4-3 tangu alipotua Old Trafford, Novemba mwaka jana.
Hata hivyo, fomesheni hiyo imeshindwa kufikia malengo yanayopaswa na jambo kubwa likielezwa ni kukosekana kwa wachezaji wanaofiti kwenye mfumo.
Amad Diallo na Diogo Dalot ndiyo walianza kutumiwa na kocha Amorim kwenye nafasi ya wing-back ya kulia na kushoto tangu alipotua kwenye klabu hiyo.
Lakini, kwa sasa Amad anatumika zaidi kwenye eneo la kushambulia huko Dalot akionekana bado anateseka na mfumo huo, jambo linalomfanya kocha Amorim kutafuta machaguo mengine ili kupata suluhisho. Na kwenye hilo, Amorim macho yake yameangukia kwa beki wa kushoto wa Lecce, Dorgu kwenye dirisha hili la uhamisho wa Januari na inavyoripotiwa dili hilo lipo kwenye hatua za mwisho kabisa kukamilika.
Man United iliripotiwa kufikia makubaliano ya kulipa Pauni 29 milioni kwenye klabu hiyo ya Serie A ili kupata huduma ya Dorgu. Na dau hilo litaongezeka Pauni 4 milioni endapo kama Man United itafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na kama Dorgu atafikisha idadi ya mechi fulani kwenye Ligi Kuu England.
Kama atatua Man United, Dorgu anaweza kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Amorim.
Ukilinganisha na takwimu za mastaa wa Man United, Amad, Dalot na Noussair Mazraoui, Dorgu, 20 ameshinda bato za ana kwa ana nyingi na kurudisha mpira kwenye umiliki wa timu yake mara nyingi msimu huu, huku akipora mipira kutoka miguuni kwa wapinzani mara nyingi, krosi nyingi na kunasa pasi za wapinzani mara nyingi kuliko wakali hao walipo Old Trafford kwa sasa.
Beki huyo wa kushoto amepiga mashuti 36 - ikiwa ni mengi kuliko wachezaji hao wengine wa Man United. Dorgu mtindo wake wa uchezaji unaonekana utaifanya Man United kuwa imara zaidi kuliko wachezaji wa sehemu ya ulinzi waliopo kwenye kikosi hicho. Ni mjuzi wa kwenda mbele kushambulia na kurudi nyuma kukaba kitu ambacho ndicho Amorim anachohitaji wachezaji wake wa pembeni wafanye.
Kitu kingine chenye faida zaidi kwa Man United kwa mchezaji Dorgu ni kuhusu ufiti wake. Mkurugenzi wa ufundi wa Nordsjaelland, Alexander Riget, mtu ambaye ameshuhudia beki huyo akiwa anakua kwenye klabu hiyo, hivi karibuni aliiambia Sport Witness: “Hajawahi kuwa majeruhi – daima.
“Aliichezea Nordsjaelland kwa miaka sita au saba na sikumbuki hata siku moja alikuwa majeruhi, kitu ambacho si cha kawaida. Hicho ni kitu kizuri.”
Habari hizo zitakuwa njema kwenye sikio la Amorim kutokana na kuwa na wachezaji wengine wa eneo hilo kuwa majeruhi mara nyingi kwa miaka ya hivi karibuni, akiwamo Tyrell Malacia na Luke Shaw. Dorgu ana uwezo mkubwa pia kwenye kufunga mabao, ambapo ushahidi ni lile bao lake alilofunga kwenye mechi yake ya kwanza ya soka la kimataifa alipoichezea Denmark, Septemba mwaka jana. Alitikisa nyavu kwenye mpira wake kwanza kugusa baada ya kuingia uwanjani tu katika dakika 42 dhidi ya Uswisi akiwa ametokea benchini. Na kama usajili wake utafiti, basi atakuwa mchezaji wa kwanza kutua Man United kwenye zama za Amorim. Man United ipo pia kwenye hatua za mwisho za kumsajili kinda wa Arsenal, Ayden Heaven.