Sikia! Florian Wirtz njia nyeupe dili la Man City
Muktasari:
- Wirtz mwenye umri wa miaka 21, alikuwa akihusishwa kuondoka Leverkusen tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu baada ya kuonyesha kiwango bora akiiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa wa Bundesliga.
MANCHESTER City imepata matumaini makubwa ya kumsajili kiungo wa Bayer Leverkusen na Ujerumani, Florian Wirtz kaitka dirisha la majira ya kiangazi mwakani baada ya Mkurugenzi wa Mtendaji wa Leverkusen kuthibitisha kwamba itakuwa ngumu kumbakisha staa huyo.
Wirtz mwenye umri wa miaka 21, alikuwa akihusishwa kuondoka Leverkusen tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu baada ya kuonyesha kiwango bora akiiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa wa Bundesliga.
Hata hivyo, ilikuwa ngumu kuondoka na akasalia lakini kwa sasa ripoti zinaeleza hadi yeye mwenyewe ameshawaambia mabosi wa timu yake kwamba anataka changamoto nyingine msimu ujao.
Man City na Bayern Munich ni miongoni mwa timu zinazomhitaji na zote zimeshaanza harakati za kumsajili.
REAL Madrid imepanga kuzungumza na wawakilishi wa beki wa Liverpool, Virgil van Dijk, 33, kwa ajili ya kuboresha eneo lao la ulinzi ikiwa hatosaini mkataba mpya hadi kufikia mwisho wa msimu.
Mkataba wa sasa wa Van Dijk unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hakuna makubaliano yoyote kati yake na mabosi wa Liverpool juu ya suala la mkataba mpya wa beki huyo kisiki Anfield.
REAL Madrid imeingia katika vita dhidi ya Bayern Munich, Manchester United na Manchester City ili kuipata saini ya beki wa kulia wa Bayer Leverkusen na Uholanzi, Jeremie Frimpong, 24, katika dirisha lijalo.
Moja kati ya mambo ambayo yanadaiwa kusababisha Madrid wahitaji huduma ya fundi huyu ni kujiandaa na maisha bila ya Dani Carvajal ambaye amekuwa akisumbuliwa sana na majeraha katika misimu ya hivi karibuni.
EVERTON ipo katika hatua nzuri kwenye mazungumzo na wawakilishi wa straika wa Rangers na Morocco, Hamza Igamane ambaye inataka kumsajili katika dirisha lijalo.
Everton huenda ikawapoteza mastaa wao Dominic Clevert Lewin na Beto mwisho wa msimu. Hamza msimu uliopita alicheza mechi 23 za michuano yote na kufunga mabao saba akiwa ASFAR ya Morocco.
TOTTENHAM ni moja kati ya timu zinazohitaji huduma ya beki kisiki wa Paris St-Germain na Slovakia, Milan Skriniar, 29, ambaye ameruhusiwa kuondoka katika dirisha lijalo ikiwa atapata timu ya kwenda.
Skriniar sio mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha PSG kwa msimu huu hali inayosababisha mabosi wa timu hiyo wamruhusu kuondoka ili kuacha nafasi wengine.
ARSENAL inadaiwa kuanza mazungumzo na wawakilishi wa kiungo wa Sevilla na Ufaransa, Lucien Agoume, 22, ambaye inamwangalia kama mbadala wa Thomas Partey.
Partey haonekani kuwa na muda mrefu wa kusalia kwenye timu hiyo kwani licha ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu, hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote juu ya kumuongeza dili jipya.
MPANGO wa Manchester City kumsajili kiungo wa Newcastle United na Brazil, Bruno Guimaraes, 27, katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani huenda ukafeli na badala yake matajiri hao wa Jiji la Manchester wanataka kuwekeza nguvu zao zaidi kwa kiungo wa Real Sociedad, Mhispania, Martin Zubimendi, 25.
KIUNGO wa AC Milan na Uholanzi, Tijjani Reijnders, 26, huenda akaendelea kusalia katika viunga vya San Siro kwa muda mrefu zaidi licha ya ripoti kuelezwa kwamba kwamba Manchester United inahitaji saini yake.
Staa huyu yupo katika hatua za mwisho kusaini mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2028.