Real Madrid yamfungia kazi Vinicius Jr
Muktasari:
- Vinicius ambaye msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote na kufunga mabao 16 ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Madrid.
WAWAKILISHI wa Mshambuliaji wa Real Madrid na Brazil, Vinicius Jr, 24, wapo katika mazungumzo na mabosi wa timu hiyo kwa ajili ya kumuongeza mkataba wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Vinicius ambaye msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote na kufunga mabao 16 ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Madrid.
Mabosi wa timu hiyo wanataka kumwongeza mkataba kwa sababu hivi karibuni baadhi ya vigogo wa Saudi Arabia ikiwemo Al-Hilal wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kutaka kumsajili na walionyesha nia zaidi kwa sababu mkataba wake sio mrefu sana.
Licha ya mazungumzo kutofikia mwafaka, ripoti zinadai kuna uwezekano mkubwa wa staa huyu kusaini dili jipya litakalompa mshahara mnono zaidi.
MANCHESTER United imepanga kumsajili mshambuliaji wa Ipswich Town raia wa England, Liam Delap, 21, ikiwa itashindwa kupata huduma za mastraika wawili iliowaweka kwenye rada zao ambao ni pamoja na Viktor Gyokeres, 26, kutoka Sporting Lisbon na staa wa kimataifa wa Nigeria na Napoli, Victor Osimhen, 26, ambaye kwa sasa anaichezea kwa mkopo Galatasaray. Mkataba Delap unatarajiwa kumalizika mwaka 2029 na anawindwa pia na vigogo wengi Ulaya ikiwamo Manchester City
MANCHESTER City imepanga kuboresha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao na mmoja kati ya mastaa ambao inataka kuwasajili ni kiungo wa Atalanta, raia wa Brazil, Ederson, 25, ambaye amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Tangu kuanza kwa msimu huu Ederson amecheza mechi 33 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
ARSENAL inataka kiasi cha pesa kitakachovunja rekodi ya dunia ya usajili wa beki ikiwa Real Madrid inahitaji saini ya beki wao wa kati, William Saliba, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Saliba ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, amekuwa akihusishwa na Madrid tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Msimu huu amecheza mechi 33 za michuano yote na kufunga mabao mawili.
BORUSSIA Dortmund huenda ikalazimika kumuuza winga wao raia wa England, Jamie Gittens, 20, ambaye anawindwa na vigogo wa Ligi Kuu England, Liverpool, Manchester United na Chelsea dirisha lijalo. Uwezekano wa Gittens kuuzwa unadaiwa ni mkubwa ikiwa Dortmund itashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Mkataba wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
KIUNGO wa Crystal Palace, raia wa England, Adam Wharton, 21, pamoja na kiungo wa Southampton na England, Tyler Dibling, 18, ni miongoni mwa mastaa wawili wanaowindwa na Tottenham dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu ili kuboresha kikosi chao baada ya kufanya vibaya kwa msimu huu. Dibling na Wharton ni kati ya mapendekezo ya kocha Ange Postecoglu.
ARSENAL imefikia hatua nzuri kwenye mazungumzo na wawakilishi wa mastaa wao Ethan Nwaneri, 17, na Myles Lewis-Skelly, 18, walioonyesha kiwango bora baada ya kupandishwa kikosi cha timu ya wakubwa Julai mwaka jana. Tangu kuanza kwa msimu huu, Nwaneri amecheza mechi 22 za michuano yote na kufunga mabao saba sawa na Myles.
STRAIKA wa Bayer Leverkusen, Victor Boniface, 24, hatoondoka tena kwenye timu hiyo hadi mwisho wa msimu licha ya kuwekewa ofa nono na matajiri wa Al Nassr ya Saudi Arabia iliyohitaji kumsajili tangu Januari. Boniface msimu huu amecheza mechi 15 za michuano yote na kufunga mabao nane. Mkataba wake unamalizika mwaka 2028.