Rashford awachanganya Wasaudia, wampa ofa nono
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Daily Mail, Rashford amekataa ofa inayofikia Pauni 35 milioni kama mshahara kwa msimu.
MSHAMBULIAJI wa Manchester United na England, Marcus Rashford, 27, ameripotiwa kukataa ofa tatu kutoka Saudi Arabia ambako timu kibao zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili.
Kwa mujibu wa Daily Mail, Rashford amekataa ofa inayofikia Pauni 35 milioni kama mshahara kwa msimu.
Rashford amekataa ofa hizo kwa sababu bado anahitaji kuendelea kusalia Ulaya kucheza soka la kiushindani.
Ripoti za Rashford kuondoka katika dirisha hili zimeibuka baada ya kocha Ruben Amorim kumuondoa katika kikosi cha kwanza tangu Desemba, mwaka jana, akidai haridhishwi na ufanisi wake kuanzia mazoezini.
Mbali ya Saudi Arabia, staa huyo anahusishwa na vigogo mbalimbali Ulaya wakiwamo PSG na Arsenal.
Rashford mwenyewe amethibitisha kwamba yupo tayari kundoka katika dirisha hili kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya kwingineko. Timu za Saudi Arabia zinazomtaka ni Al-Ahli, Al Ittihad na Al Qadsia
MSHAMBULIAJI wa Athletic Bilbao, Nico Williams, 22, yupo kwenye rada za Arsenal ambayo ipo tayari kulipa Pauni 48 milioni kwa ajili ya kuvunja mkataba wake uliosalia.
Nico aliwahi kuhusishwa na Barcelona katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, lakini ilishindikana ikielezwa kwamba klabu hiyo ingerudi msimu ujao. Mkataba wa Nico na Bilbao unatarajiwa kumalizika 2027.
CHARLOTTE FC ya Marekani ipo katika hatua za mwisho kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa Newcastle United na Paraguay, Miguel Almiron, 30, katika dirisha hili la usajili kwa ada ya uhamisho ya Pauni 16 milioni.
Almiron anadaiwa kuomba kuondoka Newcastle ili kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine baada ya kocha Eddie Howe kuonyesha hana mpango naye tangu mwanzo wa msimu huu.
JUVENTUS inaitaka huduma ya beki wa kushoto wa Manchester United na Uholanzi, Tyrell Malacia, 25, kwa mkopo wa nusu msimu utakaodumu hadi mwisho wa msimu huu.
Malacia hajapata nafasi ya kutosha kucheza katika kikosi cha kwanza cha Man United huku tatizo la majeraha ya mara kwa mara likimuathiri.
Mkataba wa sasa wa staa huyo unatarajiwa kumalizika Juni, 2026.
TOTTENHAM Hotspur huenda ikaachana na mpango wa kumsajili beki wa kushoto wa Lecce, Patrick Dorgu, 20, baada ya timu hiyo kuongeza bei ikitaka karibu Pauni 30 milioni.
Staa huyo wa kimataifa wa Denmark ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Lecce.
Kwa sasa Dorgu anahusishwa sana kutaka kuondoka.
MANCHESTER United inaangalia uwezekano wa kuachana na winga raia wa Brazil, Antony Matheus dos Santos maarufu kama Antony katika dirisha hili ambapo Real Betis inatajwa kuwa na mpango wa kutaka kumsajili kwa mkopo. Antony sio mmoja kati ya wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Man United na inaelezwa kocha wa timu hiyo hayupo katika mipango yake.
BBEKI wa kati wa AC Milan na England, Fikayo Tomori, 27, amewaambia wawakilishi wake anataka kusalia kupambania nafasi kikosi cha kwanza licha ya Juventus kuonyesha nia ya kumtaka. Fikayo aliyekuwa miongoni mwa mastaa tegemeo AC Milan msimu uliopita, huu hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza.
FIORENTINA inajaribu kufikia makubaliano na Liverpool ili kuipata saini ya winga wa timu hiyo na Italia, Federico Chiesa, 27, katika dirisha hili. TuttoMercato imeripoti kuwa Fiorentina imeandaa ofa ya Pauni 5.8 milioni ili kumpata staa huyo ambaye amekuwa akipitia kipindi kigumu tangu ajiunge na Liverpool majira ya kiangazi mwaka jana.