Osimhen kuwa mbadala wa Salah Liverpool
Muktasari:
- Mabosi wa Liverpool walitaka kumsajili Osimhen, 25 kujiandaa na maisha bila Mohamed Salah ambaye mkataba unamalizika mwisho wa msimu huu. Salah anahusishwa na timu nyingi za Saudi Arabia tangu majira ya kiangazi 2023.
LIVERPOOL ilikuwa ni moja kati ya timu zilizotaka kumsajili mshambuliaji wa Napoli na Nigeria, Victor Osimhen katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini ilishindikana baada ya kutaka mshahara mkubwa.
Mabosi wa Liverpool walitaka kumsajili Osimhen, 25 kujiandaa na maisha bila Mohamed Salah ambaye mkataba unamalizika mwisho wa msimu huu. Salah anahusishwa na timu nyingi za Saudi Arabia tangu majira ya kiangazi 2023.
Ikiwa Osimhen hatapata timu hadi Januari mwakani na Salah asiposaini mkataba mpya kuna uwezekano Liverpool ikarudi tena mezani na wawakilishi wa Osimhen ili kuangalia namna ya kumpata.
Liverpool haionekani kuwa na shida ya kutoa ada ya uhamisho inayohitajika na Napoli lakini inakwama mshahara, ila ikimuuza Salah inayemlipa Pauni 400,000 kwa wiki inaweza kukamilisha dili kwa kuwa itakuwa imeshapunguza bili ya mishahara.
Wakati huo huo mabosi wa Newcastle United wamekanusha taarifa zinazodai kwamba beki wa kulia, Kieran Trippier huenda akatimkia Saudi Arabia au Uturuki ambako kuna timu kibao zinazotaka huduma yake. Trippier mwenye umri wa miaka 33, bado ana mkataba wa kuendelea kuitumika Newcastle hadi 2026, lakini taarifa zinaeleza ana ofa nono kutoka nchi tajwa.
MANCHESTER United inatazamia kumsajili beki wa Fulham na Marekani, Antonee Robinson, 27, katika dirisha lijalo la majira ya baridi. Taarifa zinaeleza kocha Erik Ten Hag alivutiwa na kiwango alichoonyesha staa huyo katika mechi za mwanzoni mwa msimu na ifikapo Januari kuna uwezekano wakamsajili ingawa bei yake haitapungua Pauni 30 milioni.
SEVILLA imejiondoa katika vita ya kuwania saini ya mshambuliaji wa zamani wa Atletico Madrid, Mholanzi Memphis Depay, 30, baada ya staa huyo kutaja dau kubwa la mshahara analotaka. Depay kama ilivyo kwa wachezaji wengine waliokuwa huru kabla ya dirisha kufungwa dirisha la usajili wanaruhusiwa kusajiliwa na timu yoyote Ulaya.
WINGA wa zamani wa Chelsea na Fulham, Willian, 36, anadaiwa kuwasili Ugiriki ambako amekwenda kumalizana na Olympiakos inayotaka kumsajili. Kwa mujibu wa mwandishi mbobezi wa usajili Fabrizo Romano, Willian na Olympiakos walishafikia makubaliano na staa huyo ametua nchini humo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mwisho za usajili.
ROMA ipo katika mpango wa kutaka kumsajili beki wa kati kutoka Ujerumani, Mats Hummels ambaye yupo huru baada ya mkataba wake na Borussia Dortmund kumalizika msimu uliopita. Roma inataka kumsajili Hummels ili akazibe pengo la Chris Smalling, 34, anayetarajiwa kuondoka kwenda kujiunga na Al-Fayha ya Saudi Arabia.
ROMA imeripotiwa kuwa katika hatua za mwisho kuipata saini ya beki wa zamani wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Mario Hermoso, 29, ambaye kwa sasa yupo huru baada ya mkataba wake na Atletico kumalizika kwenye dirisha lililopita. Mabosi wa Roma wanataka kuboresha eneo la ulinzi ambalo lilikuwa na upungufu msimu uliopita na huenda nyota ya mchezaji huyo ikaibukia katika mitaa ya Jiji la Roma msimu huu.
BEKI wa Newcastle United na timu ya taifa ya Ireland ya Kaskazini, Jamal Lewis, 26, yupo katika hatua za mwisho mwisho kujiunga na Sao Paulo ya Brazil. Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya Belfast Telegraph, Lewis ameshatua Brazil kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya na taratibu nyingine za usajili kabla ya kukamilisha dili hilo. Nyota huyo hana namna kikosini.