Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Neymar anataka kutimkia Brazil, kutua Santos

Muktasari:

  • Neymar ambaye tangu atue Hilal hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa kutokana na majeraha ya mara kwa mara anayoyapata, pia yupo tayari kupunguza mshahara wake hadi kufikia robo ili kukamilisha dili hilo.

MSHAMBULIAJI wa Al-Hilal, Neymar, 32, anataka kuachana na timu hiyo katika dirisha hili na kurudi Brazil kujiunga na Santos ambayo ni timu yake ya utotoni.

Neymar ambaye tangu atue Hilal hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa kutokana na majeraha ya mara kwa mara anayoyapata, pia yupo tayari kupunguza mshahara wake hadi kufikia robo ili kukamilisha dili hilo.

Staa huyu sio sehemu ya mipango ya kocha wa sasa wa Al-Hilal, Jorge Jesus ambaye hajamjumuisha katika orodha ya mastaa wanaotakiwa kucheza ligi kwa mechi za mzunguko wa pili.

Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi mbili tu ambazo pia aliingia akitokea benchini.

Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na inadaiwa ameshafanya uamuzi kwamba anataka kurudi Brazil na kuichezea Santos.

Al Hilal imempa machaguo mawili aidha akubali kutolewa kwa mkopo na kupunguziwa mshahara wake wa Pauni 2.5 milioni anaoupata sasa au mkataba wake uvunjwe kabisa.


RAIS wa Lecce, Sticchi Damiani ameweka wazi kwamba wamepokea ofa kutoka Manchester United inayohitaji saini ya beki wao wa kushoto, Patrick Dorgu, 20, katika dirisha hili.

Inaelezwa Lecce haitaki kumuuza fundi huyu kwa sasa lakini hilo linaweza kutokea mwisho wa msimu.

Hata hivyo, inaweza kushawishika kumuuza Januari hii lakini kwa timu itakayokuwa tayari kuweka ofa nono mezani.


KIUNGO wa Aston Villa na Argentina, Emiliano Buendia, 28, amefikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja wa kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2027.

Staa huyu anayewindwa na timu mbalimbali barani Ulaya ikiwamo zile za kutoka Saudi Arabia, Italia na Ujerumani, mkataba wake wa awali unatarajiwa kumalizika Juni mwaka 2026.


BEKI wa Chelsea, Mfaransa Axel Disasi, 26, ni miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na Aston Villa na timu hiyo imepanga kumsajili kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Disasi ni mmoja kati ya wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Chelsea na alihitaji kuondoka tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana. Villa inahitaji kumchukua hata kwa mkopo.


MSHAMBULIAJI wa RB Leipzig ambaye anacheza kwa mkopo Tottenham, Timo Werner, 28, pamoja na wawakilishi wake wapo katika mazungumzo na New York Red Bull ya Marekani kwa ajili ya kujiunga nayo katika dirisha hili.

Werner ni miongoni mwa mastaa ambao hawapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Spurs chini ya Ange Postecoglu hali inayosababisha afikirie kuondoka.


BEKI na kapteni wa Liverpool, Virgil van Dijk hana uhakika kama ataendelea kusalia kwenye viunga vya timu hiyo au ataondoka mwisho wa msimu huu.

Kwa mijibu wa ripoti, Van Dijk amepokea ofa kutoka timu nyingi za Ulaya na Saudi Arabia ambazo zinatamani kumsajili mwisho wa msimu ambapo mkataba wake utakuwa unamalizika.

Hadi sasa wawakilishi wa fundi huyu na Liverpool hawajafikia mwafaka juu ya suala la mkataba mpya.


AC Milan inataka kuwasilisha ofa inayofikia Euro 33 milioni hadi Euro 34 milioni kwenda Feyenoord ili kuipata saini ya straika wa timu hiyo na Mexico, Santiago Gimenez, 23, katika dirisha hili.

Hata hivyo, ofa hiyo ina nafasi ndogo ya kufanikiwa kwa sababu haijafikia kiwango ambacho Feyenoord inakihitaji.

Kwa mujibu wa tovuti ya Calciomercato timu hiyo inahitaji kuanzia Euro 40 milioni ili kumuuza Gimenez.


SOUTHAMPTON inataka kusikiliza ofa kwa ajili ya kumuuza beki wake Kyle Walker-Peters katika dirisha hili. Fundi huyu ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu ameshaanza kupokea ofa kutoka timu mbalimbali ikiwamo Galatasaray. So’ton inataka kumuuza kwa sababu amekataa kusaini mkataba mpya, hivyo inahofia kuona akiondoka bure.