NDINGA KALI: Kwenye magari Salah ni habari nyingine
Muktasari:
- Mohamed Salah ni mmoja wa mastaa wanaopenda magari ya kifahari na kwenye eneo lake la maegesho, ameweka magari mbalimbali anazozimiliki na hapa tunakueleza aina, uwezo na thamani yake.
LIVERPOOL, ENGLAND: WACHEZAJI wengi wa soka wanapenda starehe na kununua vitu mbalimbali vya thamani kama saa, boti, nyumba, vito na wengine magari.
Mohamed Salah ni mmoja wa mastaa wanaopenda magari ya kifahari na kwenye eneo lake la maegesho, ameweka magari mbalimbali anazozimiliki na hapa tunakueleza aina, uwezo na thamani yake.
5. Bentley Continental GT
Anamiliki mawili ya aina hii na yanakadiriwa kuwa na thamani ya Pauni 160,000 kila moja.
Ndani yake ina mandhari mazuri ikiwa ni pamoja na viti vya ngozi vyenye nakshi na ina kasi ya karibia kilomita 210 kwa saa, pia ina injini ya V12.
Mashabiki wengi wanalijua gari hili na wanapoliona baadhi huwa wanalikimbilia kwa ajili ya kupata picha na staa huyo.
4. Bentley Bentayga
Moja ya magari ya kifahari zaidi lenye milango minne. Ilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015 na ikawa gari linalotakiwa sana na wachezaji wa soka wengi duniani kote.
Mbali ya Salah, Kyle Walker na Raheem Sterling pia wanalimiliki.
Mwaka 2016 yalikuja likiwa na injini kubwa ya twin-turbo W12 na yalikuwa yanauzwa kuanzia Pauni 170,000.
3. Porsche 911 Turbo S
Gari hili la kifahari aina ya 911 Turbo S, injini yake ina turbo mbili. Gari hili linakimbia kilomita 205 kwa saa na ndilo lenye kasi zaidi kuwahi kutengenezwa na kampuni ya Porsche na hadi sasa bado anamiliki gari hili. Bei yake inakaribia Pauni 100,000.
2. Lamborghini Aventador
Kama ilivyo kwa mastaa wengi wa soka, Salah pia ana Lamborghini Aventador katika maegesho yake lenye uwezo wa kufikia kasi ya juu ya kilomita 218 kwa saa na ndilo lenye kasi zaidi analomiliki kwa sasa, kwa mujibu wa taarifa mbalimbali gari hili bei yake inaanzia Pauni 270,000 hadi 500,000.
1. Mercedes-Benz AMG GLE Coupe
Wachezaji wengi wanapoenda mazoezi hupendelea kuendesha gari lenye nafasi ya kutosha ndani.
Hii ndiyo sababu wengi wao wanamiliki magari kama Range Rovers na Bentley Bentayga.
Kwa upande wa Salah anamiliki ndinga hii ambayo thamani yake dukani inafikia Dola 129,050.
Gari hili amekuwa akilitumia zaidi kwenda mazoezini na ameonekana nalo mara kadhaa.
Mbali ya hayo pia ana Mercedes-Benz SLS AMG Roadster ambalo ni moja kati ya magari ya bei ya juu ambayo kampuni ya Mercedes imewahi kuyaingiza sokoni, lakini hiyo haikumzuia Salah kulinunua mwaka 2022.
Ndinga hii ina uwezo wa kukimbia kwa kasi ya kilomita 197 kwa saa moja. Bei yake ni Pauni 175,000.
Fundi huyu pia anamiliki ndinga la kifahari aina ya Audi Q7, ambalo mastaa wengi wamekuwa wakitumia.
Salah aliinunua aliporejea England kujiunga na Liverpool akitokea Roma mwaka 2017.
Wachezaji wengi maarufu wa Barcelona walitumia Q7 kwenda na kurudi mazoezini waliyopewa kama sehemu ya mkataba wa kampuni hiyo na Barca. Bei ya gari hili inaanzia Pauni 67,000.