Man United kutoa pesa, Hojlund ili imbebe Osimhen
Muktasari:
- Ripoti zinafichua Man United imechoshwa na kiwango cha Hojlund, hivyo kwa sasa inataka kuachana naye, lakini itamtumia kama chambo kwa Osimhen ili aje kwenye kikosi chao kwa ajili ya msimu wa 2025/26.
MANCHESTER United imeripotiwa kuwa na mpango wa kutoa Pauni 33 milioni pamoja na mshambuliaji Rasmus Hojlund ili kumchukua straika wa Kinigeria, Victor Osimhen dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Ripoti zinafichua Man United imechoshwa na kiwango cha Hojlund, hivyo kwa sasa inataka kuachana naye, lakini itamtumia kama chambo kwa Osimhen ili aje kwenye kikosi chao kwa ajili ya msimu wa 2025/26.
Thamani ya Osimhen ni Pauni 62 milioni, lakini Man United haipo tayari kulipa kiasi chote hicho cha pesa na ndiyo maana imepanga kumtumia Hojlund kwenye dili hilo, wakiamini Napoli watakubali mpango huo. Osimhen kwa sasa anacheza kwa mkopo huko Galatasaray ya Uturuki hadi mwisho wa msimu huu.
Marcus Rashford
MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Marcus Rashford ameripotiwa kuwa na mpango wa kuachana jumla na timu yake hiyo mwishoni mwa msimu baada ya sasa kucheza kwa mkopo Aston Villa. Barcelona na Bayern Munich nazo zinahitaji saini ya mchezaji huyo ili akakipige kwenye timu zao msimu ujao. Fowadi huyo wa England anapiga hesabu za kuachana na Man United, huku Aston Villa iweza kumchukua kwa Pauni 40 milioni.
Alexander Isak
LIVERPOOL imeripotiwa kuwa na mpango wa kumsajili straika wa Newcastle United na Sweden, Alexander Isak dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Mpango huo wa Liverpool unaweza kuwaingiza kwenye vita kali na Arsenal na kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na mshambuliaji huyo ikihitaji aende akaboreshe safu yao ya ushambuliaji ili iwe timu ya kushindania mataji msimu ujao.
Leandro Trossard
ARSENAL imeripotiwa kuweka wazi milango ya kumpiga bei winga wao, Leandro Trossard kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya. Arsenal inataka kumuuza winga huyo wa Kibelgiji mwenye umri wa miaka 30 ili kufungua njia ya kufanya usajili wa wachezaji wengine wa kuja kujenga kikosi hicho na kuwa na kibingwa ndani ya uwanja.
Karim Adeyemi
CHELSEA imeripotiwa kuwa na mpango wa kumsajili winga wa Borussia Dortmund, Karim Adeyemi dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Chelsea inahitaji kuongeza nguvu kwenye safu yake ya ushambuliaji hasa kwa upande wa pembeni, hivyo inamtazama Mjerumani huyo kuwa mchezaji anayewafaa zaidi, huku thamani yake ikithaminishwa kuwa Pauni 37 milioni, ambayo ni pesa ndogo kwa matajiri hao wa Stamford Bridge.
Diogo Costa
MANCHESTER City inaripotiwa kuwa na mpango wa kusajili kipa mpya kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku macho yao yakiangukia kwa mkali wa FC Porto, Diogo Costa. Mabosi wa Etihad wanaamini kipa huyo wa kimataifa wa Ureno ana vigezo vyote vinavyofaa kwenye kumbadili Mbrazili Ederson, 31, kwenye kikosi chao wakati wa dirisha lijalo la usajili.
Joshua Kimmich
BAYERN Munich imeripotiwa kuondoa ofa yao mezani kwa kiungo wa Kijerumani, Joshua Kimmich baada ya mchezaji huyo kusuasua kusaini dili jipya. Kutokana na hilo, Kimmich ambaye mkataba wake utaisha mwisho wa msimu huu atakuwa huru kujiunga na timu yoyote bure kabisa mwishoni wa msimu. Timu kibao za Ligi Kuu England zimehusishwa na mchezaji huyo.
Rafael Leao
BARCELONA imeripotiwa kuonyesha nia na dhamira ya kunasa saini ya winga wa Kireno, anayekipiga AC Milan, Rafael Leao mwisho wa msimu. Kinachoelezwa ni Barcelona inamtazama winga huyo, 25, kama aina ya wachezaji wanaoweza kufiti kwenye kikosi chao na ndiyo maana inataka kuinasa saini yake dirisha la uhamisho majira ya kiangazi.