Madrid yasubirishwa kwa Trent Alexander-Arnold
Muktasari:
- Ripoti zinaeleza Liverpool bado ina matumaini ya kutaka kumbakisha na hawatokubali ofa yoyote kwa sasa hivyo Madrid italazimika kusubiri hadi mwisho wa msimu atakapokuwa huru.
LIVERPOOL inadaiwa kutupilia mbali ofa ya Real Madrid iliyowasilishwa katika dirisha hili kwa ajili ya kumsajili beki wao raia wa England, Trent Alexander-Arnold, 26, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Ripoti zinaeleza Liverpool bado ina matumaini ya kutaka kumbakisha na hawatokubali ofa yoyote kwa sasa hivyo Madrid italazimika kusubiri hadi mwisho wa msimu atakapokuwa huru.
Trent ambaye hadi saasa hajafikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya, msimu huu amecheza mechi 23 za michuano yote na kutoa asisti tano.
Beki huyu anaripotiwa kuwa hataki kubakia tena Liverpool na ameshafanya uamuzi wa kuondoka pale mkataba wake utakapomalizika. Mara kadhaa imekuwa ikizungumziwa ishu yake ya mkataba mpya lakini bado hajasaini.
JUVENTUS na Napoli zinapambana kuipata saini ya straika wa Manchester United na Uholanzi, Joshua Zirkzee, 23, katika dirisha hili.
Mshambuliaji huyu wa kimataifa wa Uholanzi hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa tangu ajiunge na mashetani wekundu katika dirisha lililopita na wiki iliyopita alizomewa na mashabiki wa timu yake. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 27 za michuano yote na kufunga mabao manne.
LICHA ya kusema hadharani kwamba hadi sasa hajaanza mazungumzo ya mkataba mpya, taarifa kutoka tovuti ya The Mirror zinaeleza kwamba mshambuliaji wa Liverpool na Misri, Mohamed Salah, 32, na beki wa timu hiyo, Virgil van Dijk, 33, wataongeza mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa miaka miwili.
Mikataba ya mastaa hawa inatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na Salah alisema yuko jirani zaidi kuondoka kuliko kubaki.
LIVERPOOL ipo tayari kumuuza straika wake raia wa Uruguay, Darwin Nunez, 25, katika dirisha hili na kutumia pesa itakazopata kwa ajili ya kufanya usajili wa mshambuliaji wa Inter Milan na Ufaransa, Marcus Thuram, 27, pamoja na straika wa Newcastle na Sweden, Alexander Isak, 25.
Inaelezwa, kocha Arne Slot harizishwi na kiwango chake. Mkataba wa sasa wa Nunez unaisha mwaka 2028.
MANCHESTER United na Liverpool zipo kwenye vita kali ya kumsajili beki wa kushoto wa Bournemouth na Hungary, Milos Kerkez, 21, katika dirisha hili.
Kerkez amevutia vigogo hawa kutokana na kiwango bora alichokionyesha hususani msimu huu ambapo amecheza mechi 19 za michuano yote na kufunga bao moja. Mkataba wake unamalizika mwaka 2028.
REAL Madrid imevutiwa na beki kisiki wa AFC Bournemouth na Hispania, Dean Huijsen, 19, na inahitaji kumsajili katika dirisha hili ili kuboresha eneo lao la ulinzi.
Dean ambaye msimu huu amecheza mechi 14 za michuano yote na kufunga mabao mawili, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
BAYERN Munich imewaweka katika rada makipa mbalimbali inaohitaji kuwasajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na mmoja kati yao ni kipa wa Brighton na Uholanzi, Bart Verbruggen, 22.
Munich inahitaji kusajili kipa katika dirisha lijalo kwa sababu Manuel Neuer anaweza kuondoka mwisho wa msimu huu. Mkataba wa Bart unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
CHELSEA ina mpango wa kumuuza kiungo wake raia wa Italia, Cesare Casadei, 21, ambaye yupo katika rada za Torino inayohitaji kumsajili hata kwa mkopo katika dirisha hili la majira ya baridi.
Casare, 21, mkataba wake unaisha 2028. Anahusishwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.