Liverpool yawasilisha ofa Leipzig ikimtaka Diomande
Muktasari:
- Paris St-Germain pia wanavutiwa na Diomande, ambaye ameashiria kuwa angependa kuhamia katika klabu hiyo ya Ufaransa, lakini kambi yake imekuwa ikisisitiza kwamba uamuzi utafanyika mara tu baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuanza Alhamisi, wiki ijayo huko Amerika.
INADAIWA kwamba Liverpool wamewasiliana na RB Leipzig kuhusu uhamisho wa winga wa kimataifa wa Ivory Coast, Yan Diomande ambaye amekuwa gumzo katika dirisha hili la usajili aende akawe mbadala wa Mohamed Salah ambaye ameshatimka Anfield mara tu baada ya msimu kumalizika.
Awali, ilidaiwa kwamba Liverpool walikuwa wakiwasiliana chinichini na mchezaji mwenyewe pamoja na kambi yake kwa ajili ya kuweka mambo sawa kabla ya kuibua katika timu yake ili kwenda kumalizana. Hata hivyo inadaiwa kwamba RB Leipzig imeweka msimamo wa kutomuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19.
Paris St-Germain pia wanavutiwa na Diomande, ambaye ameashiria kuwa angependa kuhamia katika klabu hiyo ya Ufaransa, lakini kambi yake imekuwa ikisisitiza kwamba uamuzi utafanyika mara tu baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuanza Alhamisi, wiki ijayo huko Amerika.
Mchezaji huyo amekuwa katikati ya mjadala wa usajili kutokana na kuwa na msimu bora katika Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga). Nyota huyo anamaliza mkataba Juni 30, 2030.
Said El Mala
ARSENAL wanakabiliwa na ushindani kutoka Paris St-Germain kwa winga wa Cologne, Said El Mala, ambaye tayari ameshaeleza kwamba hana nia ya kujiunga na Brentford ya Ligi Kuu England iliyowasilisha ofa mezani kwake kabla ya kumalizika kwa msimu wa ligi za Ulaya.
El Mala ambaye ni miongoni mwa masupastaa wa Bundesliga msimu ulioisha ameshaitaarifu timu yake kwamba hana mpango wa kusalia kikosini msimu ujao. Mkataba wake unamalizika Juni 30, 2030.
Eli Junior Kroupi
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ufaransa, Eli Junior Kroupi, 19, anayekipiga katika kikosi cha Bournemouth ameingia mzima mzima katika rada za Paris St-Germain katika dirisha hili la usajili baada ya kuonyesha makali kwenye msimu uliopita huko England.
Hata hivyo, PSG itakuwa na kazi kubwa kupambana na timu zinazomtaka nyota huyo zikiwamo Bayern Munich, Atletico Madrid na Real Betis. Mkataba anamaliza Juni 2030.
Marc Cucurella
BEKI wa Chelsea na Ufaransa, Marc Cucurella, 27, anatafakari uwezekano wa kuondoka Stamford Bridge, huku Atletico Madrid ikitarajiwa kutoa ofa ya awali kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania.
Cucurella ni mmoja wa wachezaji ambao waliushutumu uongozi wa Chelsea kuachana na kocha Enzo Maresa, Januari 2026, akiwa sambamba na nahodha msaidizi Enzo Fernandez. Mkata wake unaishi Juni 2029.
Andrea Cambiaso
JUVENTUS wanataka angalau Pauni 26 milioni kwa ajili ya beki wa pembeni raia wa Italia, Andrea Cambiaso, 26, ambaye anahusishwa na Chelsea pamoja na Barcelona.
Kwa mujibu wa Calciomercato, mchezaji huyo ameshaeleza bayana kwamba anapenda kuondoka katika timu yake ili kwenda sehemu nyingine ambako atapata nafasi kubwa ya kucheza na kunadili mazingira ya kazi.
Dusan Vlahovic
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Serbia, Dusan Vlahovic, 26, anatarajiwa kuondoka Juventus wakati mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa Juni hii, baada ya kuamua kutosaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Italia ikielezwa kwamba alitaka kuongezewa maslahi kabla ya kumwaga wino.
Mmoja wa vigogo wa klabu hiyo, Damien Jacques Comolli anadai nyota huyo alitaka kulipwa mara tatu zaidi ili asaidi dili jipya suala ambalo wameshindwa kukubaliana.
Jean-Philippe Mateta
JUVENTUS wamefufua tena nia yao kwa mshambuliaji wa Crystal Palace na Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, 28, na pia wanamvutia mshambuliaji wa Atletico Madrid na Norway Alexander Sorloth, 30.
Taarifa ya Gazzetta dello Sport inadai wachezaji hao wamewekwa katika orodha ya kwenda kuziba pengo la Dusan Vlahovic anayetarajiwa kuondoka mwishoni mwa mwezi huu.
Mateta aliwahi kuwa katika rada ya timu hiyo dirisha lililopita, lakini mpango wa kumsajili uliishia njiani.
Zadok Yohanna
AIK Stockholm inadai ipo kwenye mazungumzo ya kumuuza winga wa Nigeria mwenye umri wa miaka 18, Zadok Yohanna, ambaye anahusishwa na Brighton, Chelsea na Newcastle United.
Kwa mujibu wa Northern Echo, Yohanna amekuwa akihusishwa na timu nyingine nyingi Ulaya, lakini vigogo hao wa England wanapewa nafasi kubwa ya kuinasa saini yake, huku pia zikitajwa timu mbili za Italia ambazo ni Juventus na Inter Milan. Mchezaji huyo na AIK Stockholm mkataba wao unaisha Juni 2029.