Kumeanza kuchangamka! Monaco nayo yaingia kwenye vita kumnasa Rashford
Muktasari:
- Rashford anatarajia kuachana na timu yake kwenye dirisha hili la Januari baada ya kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kocha Ruben Amorim.
MONACO, UFARANSA: AS Monaco imeingia kwenye mbio za kumsajili Marcus Rashford huku klabu hiyo ya Ufaransa ikiwa na uhakika kwamba ina mkwanja wa kutosha wa kunasa huduma ya mshambuliaji huyo wa Manchester United.
Rashford anatarajia kuachana na timu yake kwenye dirisha hili la Januari baada ya kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kocha Ruben Amorim.
Hajacheza mechi kwenye kikosi cha kwanza kwa mwezi mzima sasa tangu alipowekwa kando kwenye mechi dhidi ya Manchester City na tangu hapo aliwekwa kando mara kadhaa kabla ya kurudi kwenye kikosi, lakini aliishia tu kwenye benchi.
Fowadi huyo yupo kwenye orodha ya wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa, lakini anacheza kwa kiwango cha chini huku mchezaji mwenyewe akifungua milango ya kwenda kukabiliana na changamoto mpya. Monaco sasa ipo tayari kumpa ofa tamu ya kumfanya akacheze kwenye Ligue 1, akaboreshe makali kwenye safu yao ya ushambuliaji ili kufukuzia ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Kocha wa AS Monaco, Adi Hutter, ambaye aliongoza timu hiyo kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, anahitaji mshambuliaji wa pembeni na ndio maana anamtaka Rashford akafanye kazi kwenye kikosi chake. Klabu hiyo ya manispaa hailipi kodi, hivyo jambo hilo linaifanya kuwa na nafasi kubwa ya kumudu mishahara ya Rashford, ambaye analipwa zaidi ya Pauni 300,000 kwa wiki.
Monaco pia ipo kwenye hatua za mwisho za kumsajili Mika Biereth, mshambuliaji wa kati kutoka Sturm Graz, lakini imepania kufanya usajili wa nyota wengi kwenye dirisha hili la Januari ili kufanya kikosi chao kuwa moto. Timu hiyo ina shika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligue 1 na ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo msimu huu ipo kwenye mtindo mpya kabisa.
Staa wa zamani wa Liverpool, Takumi Minamino na yule wa Arsena, Folarin Balogun ni sehemu ya safu ya ushambuliaji ya Monaco, lakini wawili hao wameshindwa kuwa moto msimu huu, jambo linaloifanya timu hiyo kufungua pochi ili kuleta nguvu mpya kwenye fowadi yao.
Kuhusu Rashford kumekuwa na timu nyingine pia za Italia, AC Milan na Juventus zikimtaka mchezaji huyo kwa mkopo. Borussia Dortmund nayo inaripotiwa kuwa kwenye mchakamchaka huo sambamba na Barcelona. Lakini, timu hizo zote hazina pesa ya kutosha kumudu mshahara wa mchezaji huyo, jambo ambalo linaifanya Monaco, ambayo ni timu ya manispaa kuwa kwenye nafasi nzuri ya kunasa huduma ya zao hilo la Old Trafford walau hata kwa mkopo hadi mwisho wa msimu, huku wakibeba majukumu yote ya kumlipa mshahara mchezaji huyo na kuipunguzia mzigo Man United.
Rashford atakuwepo kwa ajili ya mechi ya kuwakabili Arsenal leo Jumapili kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA.
Alipoulizwa kama Rashford bado yupo kwenye mipango ya Man United kwa ajili ya baadaye kama ataondoka kwa mkopo mwezi huu, kocha Amorim alisema: “Tutaona jamani. Acha sasa akili yetu iwe kwenye mchezo. Wachezaji wapo, wamefanya mazoezi, tutaona itakavyokuwa kwenye mechi hii.”
Man United inakaribisha ofa kwa klabu nyingine zinazotaka wachezaji wao ikiwa ni sehemu ya kujaribu kukifumua kikosi hicho ili kukijenga upya. Hakuna mchezaji ambaye hauzwi hata kwa kinda mwenye kipaji kama Kobbie Mainoo, ambaye anaripotiwa kuwa yupo kwenye mazungumzo na klabu yake baada ya kuhusishwa na klabu ya Chelsea inayohitaji saini yake.