Jorginho wa Arsenal anukia Flamengo Brazil
Muktasari:
- Jorginho anatajwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Arsenal kwani tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 20 za michuano yote na kufunga bao moja.
KIUNGO wa Arsenal na Italia, Jorge Luiz Frello Filho maarufu Jorginho, 33, yupo katika hatua za mwisho kufikia makubaliano na timu ya Flamengo inayoshiriki Ligi Kuu Brazil kwa ajili ya kujiunga nayo katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Jorginho anatajwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Arsenal kwani tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 20 za michuano yote na kufunga bao moja.
Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na alikuwa akihusishwa kuondoka tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Licha ya uwepo wa timu mbalimbali barani Ulaya zinazohitaji kumsajili kiungo huyo ambaye pia ana uraia wa Brazil na Italia, mchezaji huyo ameamua kuchagua kwenda kuichezea Flamengo kutokana na ushawishi mkubwa wa familia yake na mabosi wa timu hiyo.
Mchezaji huyo aliwahi pia kukiwasha katika timu za Chelsea, Napoli, Sambonifacese na Verona.
Mathys Tel
KABLA ya dirisha la usajili kufungwa leo, mshambuliaji wa Bayern Munich, Mathys Tel, 19, alikuwa ameshaonyesha nia ya kujiunga na Manchester United, lakini changamoto kubwa ilikuwa makubaliano baina ya timu hizo katika masuala ya ada ya uhamisho. Bayern ilikuwa inahitaji Man United imnunue au ikiwa kwa mkopo kuwepo kwa kipengele kinachoitaka kumnunua baada ya mkopo kumalizika.
Lloyd Kelly
BEKI wa Newcastle United, Lloyd Kelly, 26, anatarajiwa kusaini mkataba wa kudumu Juventus katika dirisha la majira ya kiangazi baada ya mkataba wake wa sasa wa mkopo kumalizika. Kwa mujibu wa ripoti, mkataba huo wa kudumu utaigharimu Juventus kiasi kisichopungua Pauni 20 milioni. Tangu kuanza kwa msimu huu Kelly amecheza mechi 14 za michuano yote.
Liam Delap
MANCHESTER United imeingia katika vita dhidi ya Tottenham Hotspur ili kuipata saini ya straika wa timu hiyo na England, Liam Delap. Delap mwenye umri wa miaka 21, amezivutia timu nyingi kutokana na kiwango bora alichoonyesha hususan msimu huu ambao tangu uanze amecheza mechi 24 za michuano yote na kufunga mabao tisa.
Allan Saint-Maximin
MPANGO wa Napoli kutaka kumsajili winga wa Al-Ahli, Allan Saint-Maximin kwa mkopo unadaiwa kuwa kwenye hatihati kutokana na masuala ya kiuchumi. Allan, 27, ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Fenerbahce mshahara unadaiwa kuwa ndio changamoto kwani Napoli inahitaji kumchukua kwa mkopo na Ahli inataka timu inayomhitaji kulipa karibu asilimia 70 ya mshahara wake.
Ethan Nwaneri
ARSENAL ipo kwenye mazungumzo na wawakilishi wa mastaa Ethan Nwaneri, 17, na Myles Lewis-Skelly, 18, ambao wameonyesha kiwango bora baada ya kupandishwa katika kikosi cha timu ya wakubwa Julai, mwaka jana wakitokea kikosi cha pili cha timu hiyo.Tangu kuanza kwa msimu huu, Nwaneri amecheza mechi 22 za michuano yote na kufunga mabao saba sawa na Myles.
Rayan Cherki
RAIS wa Olympique Lyon, John Textor amedai hawajafikia makubaliano yoyote na Borussia Dortmund iliyohusishwa kutaka kumsajili kiungo Rayan Cherki katika dirisha lililopita la majira ya baridi. Cherki mwenye umri wa miaka 21, mkataba wake unamalizika mwakani. Msimu huu amecheza mechi 26 na kufunga mabao matano.
Murillo
VIGOGO mbalimbali barani Ulaya bado wana mpango wa kutaka kumsajili beki kisiki wa kisiki wa Nottingham Forest na Brazil, Murillo, 22, ambaye msimu huu amekuwa mhimili mkubwa katika safu ya ulinzi ya Forest. Murillo ambaye pia anawindwa na Juventus na Chelsea, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029.