Guehi, Upamecano, Konate watajwa Real Madrid
Muktasari:
- Marc Guehi wa Crystal Palace, Dayot Upamecano anayeichezea Bayern Munich na Ibrahima Konate wa Liverpool ndio majina ambayo Madrid inayatazama kwa sasa na imevutiwa zaidi kutokana na hali ya mikataba yao.
REAL Madrid imewaweka katika rada mabeki watatu ambao inaweza kuwasajili Januari mwakani au mwisho wa msimu huu ili kuboresha safu ya beki.
Marc Guehi wa Crystal Palace, Dayot Upamecano anayeichezea Bayern Munich na Ibrahima Konate wa Liverpool ndio majina ambayo Madrid inayatazama kwa sasa na imevutiwa zaidi kutokana na hali ya mikataba yao.
Madrid inataka kufanya mabadiliko makubwa katika safu yao ya kuelekea madirisha mawili yajayo ya usajili kutokana na umri wa mabeki wao na majeraha ya mara kwa mara ambayo wamekuwa wakiyapata.
Guehi amekuwa mmoja wa mabeki wa kati bora katika Ligi Kuu England na wiki kadhaa zilizopita aliripotiwa anatamani sana kutua Madrid licha ya Liverpool kuwahi kufanya naye makubaliano binafsi dirisha lililopita kabla ya dili kufeli dakika za mwisho.
Upamecano naye ni miongoni mwa mabeki bora na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu, lakini hadi sasa amegoma kuongeza na amewaambia Bayern anataka changamoto sehemu nyingine.
Konate mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu na ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Liverpool na hadi sasa hajaongeza na ripoti zinadai anataka kuondoka.
Morgan Rogers
CHELSEA inaongoza katika mchakato wa kumsajili kiungo wa Aston Villa, Morgan Rogers mwenye umri wa miaka 23, kuelekea dirisha lijalo la majira ya baridi. Rogers alijiunga na Villa Januari 2024 akitokea Middlesbrough kwa ada ya takribani Pauni 15 milioni na tangu i huo, ameonyesha maendeleo makubwa chini ya Kocha Unai Emery na msimu huu amecheza mechi 10 za michuano yote. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Ian Subiabre
MANCHESTER City, Chelsea, Liverpool na Arsenal zipo katika vita ya kuiwania saini ya winga wa River Plate na Argentina, Ian Subiabre, mwenye umri wa miaka 18. Subiabre ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya vijana ya Argentina chini ya miaka 20, amewavutia vigogo wengi kutokana na kiwango alichoonyesha tangu msimu uliopita akiwa na River Plate. Vigogo tajwa hapo juu wanataka kuwasilisha ofa ili kumsajili dirisha dogo la Januari.
Endrick
MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Mbrazil mwenye umri wa miaka 19, Endrick, inadaiwa kuwaambia wawakilishi wake anataka kujiunga na Marseille ya Ufaransa katika dirisha lijalo licha ya kuwepo kwa ofa kutoka kwa timu kubwa za nyingi. Endrick ambaye alijiunga Real Madrid Julai 2024 akitokea Palmeiras kwa ada ya zaidi ya Euro 35 milioni anahusishwa kuondoka kwa sababu hapati nafasi ya kucheza.
Katika wiki kadhaa zilizopita Madrid ilikubali ombi lake la kutaka kuachiliwa kwa mkopo wa nusu msimu na ikaelezwa Juventus na West Ham zinamhitaji lakini sasa mchezaji mwenyewe anaonekana kuichagua Marseille.
Dusan Vlahovic
TOTTENHAM imeripotiwa kuongoza vita dhidi ya Chelsea na Manchester United kumwania mshambuliaji wa Juventus, Dusan Vlahovic, 25. Vlahovic amekuwa akihusishwa na kuondoka Juventus tangu dirisha lililopita kutokana na changamoto za kifedha za klabu hiyo. Hata hivyo, yeye mwenyewe haonekani kutamani kuondoka kwa sasa ingawa ofa nono ambazo zitawasilishwa mezani zinaweza kumshawishi.
Diego Moreira
CHELSEA inaweza kutumia kipengele cha kumrudisha kiungo wa kimataifa wa Ubelgiji, Diego Moreira, 21 anayecheza kwa mkopo Strasbourg. Staa huyu alipelekwa kwa mkopo Strasbourg dirisha lililopita ili kupata muda mwingi wa kucheza. Inaelezwa sasa, Maresca anaweza kutoa amri ya kuridishwa kwa staa huyo ifikapo Januari ili kuziba baadhi ya mapengo ambayo yametokana na majeraha ya baadhi ya wachezaji wao.
Gilberto Mora
REAL Madrid inamfuatilia kwa karibu kiungo raia wa Mexico, Gilberto Mora,17, anayeichezea Tijuana. Mora ni mmoja wa wachezaji wanaofanya vizuri Mexico kwa sasa na Madrid inamwona kama Luka Modric ajaye kutokana na uchezaji wake. Msimu huu amecheza mechi tisa za Ligi Kuu Mexico akiwa na Club Tijuana.
Cardoso Varela
TOVUTI ya Mundo Deportivo imeripoti Chelsea na Barcelona zimeanza kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mshambuliaji raia wa Ureno, Cardoso Varela mwenye umri wa miaka 16 anayechezea Dinamo Zagreb ya Ligi Kuu ya Croatia. Varela amekuwa akifuatiliwa na maskauti wengi Ulaya kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, kasi na kufunga kutokea pande zote.