Guardiola bado anamtamani Florian Wirtz

Muktasari:
- Awali Man City ilipoonyesha nia ya kumsajili, Wirtz mwenyewe ndio alikataa ofa yao na kuamua kusalia kwenye kikosi hicho.
KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola bado anahitaji saini ya kiungo wa Bayer Leverkusen na Ujerumani, Florian Wirtz, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya kushindwa kufanya hivyo katika madirisha mawili yaliyopita.
Awali Man City ilipoonyesha nia ya kumsajili, Wirtz mwenyewe ndio alikataa ofa yao na kuamua kusalia kwenye kikosi hicho.
Mabosi wa Leverkusen wanataka kumsainisha staa huyu mkataba wa mpya utakaomwezesha kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2028 lakini kutakuwa na kipengele ambacho kitamruhusu kuondoka kwa kiasi maalumu cha pesa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Teamtalk, katika mkataba huo mpya kipengele chake cha kuondoka kitakachowekwa kitaitaka timu inayomhitaji kulipa Pauni 100 milioni.
Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 34 za michuano yote, amefunga mabao 15 na kutoa asisti 12.
Pablo Barrios
CHELSEA inajiandaa kutoa Pauni 58.3 milioni kwenda Atletico Madrid ili kuipata saini ya beki kisiki wa timu hiyo na Hispania, Pablo Barrios, 21, katika dirisha lijalo la majira ya kuangazi.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Pablo amecheza mechi 24 za michuano yote. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Viktor Gyokeres
BARCELONA inawafuatilia kwa karibu washambuliaji wawili ambao ni pamoja na straika wa Sporting Lisbon na Sweden, Viktor Gyokeres, 26, pamoja na staa wa Newcastle United, Alexander Isak, 25, ikiwa ni katika mchakato wa kutaka kufanya maboresho kwenye eneo lao la ushambuliaji.
Tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Gyokeres amekuwa akiwindwa na vigogo wengi barani Ulaya kutokana na kiwango bora anachoonyesha tang kuanza kwa msimu huu.
Harry Kane
MABOSI wa Bayern Munich wana matumaini makubwa kwamba straika wao raia wa England, Harry Kane, 31, ataendelea kusalia kwenye kikosi chao kwa msimu ujao licha ya kuwepo kwa kipengele kinachomruhusu kuondoka kwa kiasi maalumu ifikapo Januari mwakano.
Kane ni mmoja kati ya washambuliaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Bayern na msimu huu amefunga mabao 28, katika mechi 28 za michuano yote.
Darwin Nunez
AL Nassr inadaiwa kuwa ilikuwa katika hatua nzuri ya kufanya mazungumzo Liverpool kwa ajili ya kumsajili straika wa timu hiyo na Uruguay, Darwin Nunez, 25, kwenye dirisha lililopita la majira ya baridi.
Hata hivyo, Liverpool ilikataa ofa hiyo kwa sababu bado yupo katika mipango ya kocha wa sasa wa Liverpool. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Martin Zubimendi
REAL Madrid imeingia katika vita dhidi ya Arsenal kwa ajili ya kuipata saini ya kiungo wa Real Sociedad na Hispania, Martin Zubimendi, 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Arsenal imekuwa ikitajwa kutaka kumsajili Zubimendi tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana lakini imeshindikana tangu wakati huo. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu huu amecheza mechi 30 za michuano yote.
Marco Asensio
ASTON Villa na Paris St-Germain hazikuweka kipengele chochote kinachoitaka Villa kumnunua mazima kiungo wa PSG, Marco Asensio, 29, ambaye ametua kwa mkopo katika kikosi cha Villa kwenye dirisha lililopita.
Asensio ambaye tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 17 za michuano yote, mkataba wake na PSG unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Alexis Saelemaekers
MABOSI wa AS Roma wanahitaji kumsainisha mkataba wa kudumu kiungo wa AC Milan na Ubelgiji, Alexis Saelemaekers, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi lakini Milan inahitaji kiasi kumwachia fundi huyo kwa sharti la kufanya mabadilishano na straika wao Tammy Abraham, 27, jambo ambalo Roma hawahitaji kuona likitokea. Mkataba wa sasa wa Alexis na Milan unatarajia kumalizika mwaka 2027.